Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva ameitaka serikali kubadili muundo wa tume hiyo ili iwe na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar.
Amesema hatua hiyo itawezesha NEC kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi, badala ya kutegemea wakurugenzi wa halmashauri (Ma-DED).
Alisema hayo mjini Dodoma wakati akikabidhi taarifa ya tathimini baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.
Tathimini hiyo imetolewa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo.
Lubuva alisema serikali ifanyie mapitio ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 292 ili kurekebisha vifungu vinavyokinzana.
“Pamoja na hayo, serikali inatakiwa kubadili muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuwa na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar, hiyo itafanya tume ifanye kazi zake kwa uhuru zaidi tofauti na sasa kazi hizo zimekuwa zikifanywa na wakurugenzi wa halmashauri,” alisema.
Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, tume iliamua kufanya tathimini kwa lengo la kupata mrejesho juu ya utekelezaji wa Uchaguzi Mkuu kutoka kwa wadau. Alisema ni mara ya kwanza kwa tume kufanya tathimini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.
“Tathimini hii imefanyika ikiwa ni mojawapo ya zoezi linalokamilisha mzunguko wa uchaguzi na kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mwingine,” alisema.
Alisema changamoto zilizojitokeza kwa mujibu wa wadau waliohojiwa ni pamoja na mpiga kura kutoruhusiwa kupiga kura katika eneo tofauti na lile alilojiandikisha.
Pia wapiga kura kushindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na kugawa mipaka ya kiutawala na majimbo ya uchaguzi, baada ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura na muda mfupi uliotolewa kujiandikisha na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura.
Alisema tathimini inaonesha katika baadhi ya maeneo, watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache, ukilinganisha na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
“Baadhi ya sababu zilizotolewa ni pamoja na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa kupiga kura kutokana na elimu ya mpigakura kutowafikia wapigakura wengi, pia wapigakura walijiandikisha katika daftari la kudumu kwa ajili ya matumizi mengine ili kupata kadi kwa ajili ya matumizi mengine na uwepo wa hofu, vitisho na vurugu siku ya kupigakura,” alisema.
No comments:
Post a Comment