Friday, 28 October 2016

Benki kuu ya Tanzania yaeleza hali halisi ya uchumi wa Tanzania Tangu Rais Magufuli kuingia Madarakani.

Image result for benno ndulu
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
alipoingia madarakani mwezi Novemba 2015 aliendeleza jitihada za kukuza uchumi wa nchi yetu kwa kuweka mkazo na kutoa maagizo kwenye maeneo kadhaa yakiwemo; kuongeza nguvu kwenye ukusanyaji wa kodi, kupiga vita rushwa, kuweka msisitizo mkubwa wa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza matumizi katika sekta za vipaumbele vya maendeleo. Aidha, kuzitaka Wizara, Wakala na Taasisi za Umma kuweka fedha zao Benki Kuu na kuhimiza kila mtu afanye kazi na kula kwa jasho lake ili kutekeleza falsafa ya ‘Hapa kazi tu’. 

Maagizo haya yamekuwa kichocheo cha ukuaji mzuri wa uchumi. Kupitia maagizo haya Benki Kuu tunaweza kuelezea mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika kipindi hiki kama ifuatavyo;
1.      Kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuelekeza matumizi katika sekta za vipaumbele vya maendeleo
·         Tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani mnamo Novemba mwaka 2015, makusanyo ya mapato yameendelea kuongezeka. Kwa mfano, kati ya Januari hadi Septemba 2016, makusanyo ya mapato ya ndani yalikuwa shilingi bilioni 11,174 ikiwa ni wastani wa shilingi bilioni 1,241.55 kwa mwezi, ikilinganishwa na wastani wa shilingi bilioni 950.22 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2015. Makusanyo ya mapato ya ndani katika 2016 yalitosheleza matumizi yote ya kawaida (recurrent) na kubakiza ziada kwa ajili ya ulipaji wa madeni ya nje (amortization) na sehemu kubwa ya matumizi kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Ukuaji wa Pato la Taifa (Real GDP)
·         Uchumi umeendelea kukua kwa kiwango kikubwa kutokana na sera nzuri za uchumi mpana (macroeconomic policies). Kasi ya ukuaji wa pato la Taifa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016, yaani Januari-Juni 2016, imeongezeka na kufikia asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Ukuaji huu umechangiwa na kukamilika kwa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na kuanza kutumia gesi katika kuzalisha umeme, usafirishaji, ukiwemo usafiri wa abiria kutumia reli na mabasi ya mwendo kasi (UDART); kuongezeka kwa matumizi ya simu za mkononi, uzalishaji wa gesi, vyuma na bidhaa zisizo za vyuma pamoja na kuimarika na kupanuka kwa huduma za kifedha. Sekta za uchumi zilizoongoza katika kasi ya ukuaji ni usafirishaji (asilimia 17.4), madini (mining and quarrying) (13.7), fedha na bima (asilimia 8.7), uzalishaji viwandani (manufacturing) (asilimia 8.3) na elimu (asilimia 8.0) kutokana na sera ya utoaji wa elimu ya msingi bila malipo iliyoanza Januari 2016. 
Mfumuko wa bei
·         Mfumuko wa bei ulibakia katika kiwango cha tarakimu moja (single digit) kutokana na sera nzuri ya fedha na ile ya bajeti pamoja na kupungua kwa bei za bidhaa duniani kote. Katika mwaka ulioishia Septemba 2016, mfumuko wa bei ulikua kwa asilimia 4.5 ikilinganishwa na asilimia 6.1 kaitka kipindi kama hicho mwaka 2015 na lengo la muda wa kati la asilimia 5.0. Kutokana na sera za uchumi mpana, pamoja na kuimarika kwa shilingi dhidi ya dola ya Marekani na bei ndogo za mafuta katika soko la dunia, mfumuko wa bei unatarajiwa kubakia karibu na lengo la kiwango cha muda wa kati cha asilimia 5.0. 
Shughuli za Serikali
·         Serikali ya awamu ya tano ilianza katika kipindi ambacho upatikanaji wa misaada ya kibajeti (GBS) ulikuwa siyo mzuri kutokana na kubadilika kwa sera za maendeleo za kimataifa (foreign development policies) katIka nchi wahisani ambapo mwelekeo ulikuwa ni kupeleka fedha za miradi moja kwa moja. Pamoja na nchi nyingi wahisani kujitoa katika kusaidia katika bajeti (GBS), Serikali ya awamu ya tano imeweza kushirikiana na wadau wa maendeleo (DPs) katika kutafuta njia mbadala za kuziba pengo hilo.
2.      Uimarishaji Wa Ukusanyaji Wa Mapato Uliendana Na Uimarishaji Wa Mazingira Mazuri ya Kibiashara
·         Sera nzuri za uchumi (macroeconomic policies) za awamu ya tano zimeendelea kukwamua na kuimarisha mazingira ya biashara.  Hii imejidhihirisha katika kuimarika kwa nakisi katika urari wa biashara (current account deficit) katika miezi tisa ya mwazo ya 2016. Nakisi ya urari wa biashara imepungua sana, kufikia dola za Marekani millioni 1,621.8 katika mwezi tisa ya 2016 kutoka nakisi ya dola milioni 3,715.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Hii ni kutokana na kuongezeka kwa mauzo ya nje ya bidhaa na huduma (utalii, dhahabu, bidhaa za viwandani), pamoja na kupungua kwa kiwango kikuwa kwa uagizaji wa bidhaa na huduma (mitaji, mafuta, chakula na bidhaa za chakula).
Thamani ya Shilingi
·         Kutokana na sera nzuri za Serikali ya Awamu ya Tano, thamani ya shilingi imebaki kuwa imara (wastani wa shilingi 2,178.6 kwa dola ya Marekani) ikilinganishwa na dola ya Kimarekani na sarafu zingine za nchi jirani na nchi washirika wa kibiashara. Kutokuyumba kwa shilingi kumechangiwa na kuimarika kwa uchumi; kuhamishwa kwa fedha za mashirika ya umma kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu; kupunguzwa kwa matumizi yasiyo ya lazima ya Serikali na kutoterereka kwa Akiba ya Fedha za Kigeni.
Akiba ya Fedha za Kigeni
·         Akiba ya fedha za kigeni imebaki kuwa imara, ikiwa ni dola za Marekani milioni 4,096.0 kufikia mwisho wa mwezi Septemba 2016, ambao ni uwezo wa kutosheleza uagizaji nje wa bidhaa na hudumu kwa kipindi cha miezi 4. Kuongezeka (kutotetereka) kwa Akiba ya Fedha za Kigeni kunatokana na manunuzi yanayofanywa na Benki Kuu kutoka kwenye soko la ndani la fedha za kigeni na mashirika ya umma. 
3.      Kuhamisha Fedha za Mashirika ya Umma kutoka katika Mabenki Binafsi kwenda Benki Kuu ya Tanzania
Serikali ya Awamu ya Tano iliagiza utekelezaji wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, hasa Sura ya 32 inayohusu utunzaji wa amana za mashirika ya umma na taasisi za serikali. Imechukua miaka tisa kuanza kutekeleza masharti ya hiyo kuhusu akaunti za Mashirika ya Umma, Idara za Serikali na Serikali za Mitaa. Kuchelewa huku, kulizifanya benki nyingi za biashara zitumie fedha hizo za umma kununua Dhamana za Serikali na Hati Fungani na hivyo kuifanya Serikali kuuziwa fedha zake yenyewe. Biashara hiyo sasa imekoma kutokana na hatua madhubuti za kuitekeleza sheria hiyo.
Hatua hizo zimewezesha kupatikana na kwa mafanikio yafuatayo:
(a)    Kufungua akaunti za amana za Mashirika ya Umma na Idara za Serikali: Kati ya Novemba 2015 hadi Oktoba 26, 2016, jumla ya akaunti 267 zenye jumla ya amana za Shilingi 206,913,915,522.06 zimefunguliwa. Aidha, baadhi ya taasisi hizo zimefungua akaunti za fedha za kigeni 131 zenye Dola 163,480,125.75, sawa na shilingi 357,694,000,000.00. Hivyo jumla ya amana zote za shilingi na fedha za kigeni za mashirika na taasisi za umma zinazotunzwa Benki Kuu ni shilingi 564,608,460,663.00
(b)   Amana za akaunti za Serikali za Mitaa: Serikali imeamua kufungua akaunti maalum kwa ajili ya kutunza amana za Serikali za Mitaa. Mradi huu umeanza kutekelezwa kuanzia mwezi Aprili 2016 na mpaka sasa jumla ya mikoa mitano imeunganishwa. Mikoa hiyo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza. Mpaka tarehe 26 Oktoba 2016, amana za halmashauri za mikoa hiyo mitano ambazo zipo Benki Kuu ya Tanzania zinafikia kiasi cha shilingi 108,387,942,351.15. Bila kukamilisha sehemu ya mradi huu, fedha hizi zingekuwa kwenye benki za biashara.
Matokeo:
·         Kwa upande Serikali;
·Kumeleta uwazi kuhusu mapato na matumizi ya mashirika hayo
·Kupungua kwa gharama za usimamizi wa ujazi wa fedha (liquidity management) kwenye mzunguko.
·         Kwa mabenki;
·kumeleta usawa katika ushindani kati ya mabenki badala ya wachache kunufaika kwa kupata amana za mashirika ya umma.
·kumeleta ubunifu kwa mabenki katika kubuni bidhaa (bank products) mbali mbali mpya ili kujiongezea amana.
·Kutokana na Sera ya Fedha ambayo ni rafiki, malengo mapana ya Serikali, ukuaji wa uchumi na ukuaji wa fedha ukuwa ndani ya malengo.
·Katika kipindi cha miezi tisa ya 2016, amana katika mabenki ya biashara zimeongeza kutoka asilimi 9.84 katika miezi tisa ya mwanzo wa mwaka 2015 na kufikia asilimia 11.59 kaitka miezi tisa yam waka 2016. Vile vile, riba za mikopo kwa mwaka mmoja zilipungua kutoka wastani wa asilimia 15.49 na kufikia asilimia 13.87
·Mwenendo huu wa riba ulipelekea kupungua kwa tofauti kati ya riba za mkopo na zile za amana kutoka wastani wa asilimia 5.92 ilivyokuwa katika miezi tisa ya mwanzo ya 2015 na kufikia wastani wa asilimia 2.28 katika miezi tisa ya 2016, ikimaanisha kupugua kwa gharama za mikopo.
 
Mafanikio mengine

4.      Mwenendo wa Sekta ya Kibenki

Katika kipindi cha kuanzia Septemba 2015 hadi September 2016, sekta ya kibenki imeendelea kukua ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa taasisi mpya za kifedha ikiwemo Benki ya Waalimu Tanzania (Mwalimu Commercial Bank Plc) na Canara Bank (Tanzania) Limited. Takwimu zinaonesha kuwa mabenki yetu ni imara na salama, yakiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha. Kufikia mwezi Septemba 2016, kulikuwa na jumla ya benki na taasisi za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu zipatazo 66 zenye matawi 750 nchini kote, ikilinganishwa na taasisi 62 zilizokuwa na matawi 715 mwezi Septemba 2015.

 Katika kipindi hicho, benki mbili - Guaranty Trust Bank Tanzania Ltd na Yetu Microfinance Bank Plc na taasisi ya fedha moja ya M Mortgages Tanzania Ltd zilipata leseni za muda.
Kiwango cha mitaji kikilinganishwa na mali iliyowekezwa (total capital to total risk weighted assets and off-balance sheet exposures) kilikuwa asilimia 19.24 kikilinganishwa na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha asilimia 12. Hali ya ukwasi, ambayo hupimwa kwa kuangalia uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi (liquid assets to demand liabilities), ulikuwa asilimia 34.18 ukilinganishwa na uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20. 
Mpaka kufikia Septemba 2016, mikopo chechefu ilikuwa wastani wa asilimia 9.06 ikilinganisha na wastani wa asilimia 6.61 ya Septemba 2015. Mikopo chechefu imeendelea kuwa ni changamoto katika sekta ya kibenki kutokana na ufanisi mdogo wa urejeshaji mikopo katika sekta ya kilimo na biashara.
Amana za wateja katika mabenki zilipungua kutoka shilingi trilioni 20.19 mwezi Oktoba 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 20.01 mwezi Septemba 2016. Miongoni mwa sababu zilizochangia kupungua kwa amana kwenye mabenki ni pamoja na uamuzi wa Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya umma kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, mikopo (loans and overdafts) iliongezeka kutoka shilingi za Kitanzania trilioni 14.48 mwezi Oktoba 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 15.74 mwezi Septemba 2016.
Jumla ya rasilimali (Total assets) za mabenki na taasisi za fedha ziliongezeka kwa asilimia 4.71 kutoka shilingi trilioni 26.57 mnamo Septemba 2015 mpaka shilingi trilioni 27.82 mwisho wa Septemba 2016. Kwa kipindi cha miezi tisa kufikia Septemba 2016, jumla ya faida baada ya kodi katika sekta ya kibenki iliongezeka kufikia shilingi trilioni 352.37 ikilinganishwa na shilingi trilioni 344.87 katika kipindi kilichoishia Septemba 2015.
Upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi umeendelea kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za malipo ya rejareja kupitia simu za mkononi, pamoja na huduma za kibenki kupitia mawakala (agent banking services). 
Mabenki yameendelea kutumika katika kutunza fedha na mitaji ya wateja na kurahisisha miamala au malipo kwa wateja wake. Ili kulinda maslahi ya wateja na amana zao, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kutunga sheria, kanuni na miongozo inayotumiwa na mabenki na kusimamia utekelezaji wake.
Katika kipindi husika, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea na jukumu  lake la kusimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.  Benki Kuu, imeendelea kuhakikisha kuwa mabenki na taasisi za fedha zina mikakati inayokidhi vigezo muhimu (minimum standards) kwa kupitia ukaguzi wa mabenki unaofanyika mara kwa mara. 

Maduka ya Kuuza Fedha za Kigeni

Idadi ya Maduka ya Kuuza Fedha za Kigeni (bureaux de change) imefikia 290 ikilinganishwa na maduka 266 yaliyokuwepo Septemba 2015. Mpaka kufikia Septemba 2016, maduka yapatayo 260 yalikuwa yanafanya biashara Tanzania Bara na 30 Tanzania Visiwani, ikilinganishwa na maduka 239 Tanzania Bara na 27 Tanzania Visiwani yaliyokuwa yanafanya biashara kufikia Septemba 2015.
Benki Kuu inasimamia  usalama, utulivu na uthabiti wa sekta ya benki Tanzania. Inalinda wateja wanaoweka amana zao kwenye mabenki na taasisi za fedha.  Mabenki yanaendelea kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza uchumi wa nchi; kuongeza ushindani kwenye sekta ya kibenki na kuzuia matumizi mabaya ya sekta ya kifedha. Benki Kuu imeendelea kupima ustahimilivu wa mabenki wakati inapojitokeza hali ambayo inaweza kuathiri mapato na mitaji ya mabenki hayo (Stess testing). Pia, husaidia katika kutoa mwelekeo wa Sera ya kifedha nchini.
Sekta ya kibenki imeendelea kushuhudia mabadiliko makubwa katika aina za huduma zitolewazo na katika njia zinazotumika kutoa huduma hizo. Mabadiliko hayo ni pamoja na; Huduma za kibenki kwa kufuata misingi ya Shariah; Huduma za kibenki kupitia wakala; Huduma za kifedha kupitia simu za mikononi na
Benki Kuu imeendelea kusimamia benki mbili za maendeleo (TIB na TADB) ili ziweze kutoa mikopo katika sekta mbalimbali na kuweza kuharakisha maendeleo hapa Tanzania.
Mfumo wa Upashanaji wa Taarifa za Wakopaji
Mfumo wa upashanaji taarifa za wakopaji umeendelea kuleta mafanikio makubwa katika kuboresha upatikanaji wa mikopo kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu, pamoja na taasisi nyingine zinazotoa mikopo(SACCOS, MFIs, Utility Companies, Car Dealers na HESLB). 

Mfumo huo unajumuisha utaratibu wa kuweka taarifa za wakopaji kupitia Benki Kuu (Credit reference databank), na makampuni binafsi yaliyoruhusiwa kubadilishana taarifa za wakopaji na mabenki na taasisi nyingine zinazotoa mikopo. Kufikia Septemba 2016 jumla ya wakopaji waliokuwa katika mfumo huo walikuwa zaidi ya 1,600,000 ikilinganishwa na zaidi ya 900,000 ya Septemba 2015.  

Jumla ya mikopo mpaka kufikia Septemba 2016 ilikuwa ni zaidi ya 3,000,000 ukilinganisha na zaidi ya 1,690,000 ya Septemba 2015. Katika taarifa ya mazingira ya biashara (World Bank Doing Business Report, 2017), Tanzania imefanya vizuri kutoka nafasi ya 152 hadi 44 kati ya nchi  190 zilizofanyiwa utafiti huo.
Mifumo ya Malipo Nchini
Benki Kuu imeendelea na kazi yake ya kisheria ya kusimamia mifumo ya malipo nchini ambapo Sheria ya Mifumo ya Malipo Nchini 2015 imeanza kufanya kazi. Chini ya sheria hii zimeanzishwa kanuni mbili za uendeshaji wa mifumo. Kanuni hizo ni pamoja na Kanuni ya Leseni na Vibali kwa Watoa Huduma za Mifumo ya Malipo 2015 pamoja na Kanuni za Kutoa Fedha za Kielektroniki 2015.  Uwepo wa Sheria umeimarisha usalama katika mifumo ya malipo nchini na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mifumo ya malipo ya taifa.
Kwa kipindi hiki, huduma za fedha jumuishi (financial inclusion) imeongezeka kwa kiasi kikubwa ikichangiwa na usalama uliopo kwenye mifumo ya malipo. Aidha, idadi ya watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya mtandao imeendelea kuongezeka kwa kasi kubwa. 

Kutokana na maendeleo haya, wananchi wamefaidika kwa kupata huduma mbali mbali za kifedha kama vile, kutuma na kupokea, kutunza fedha, huduma za bima, huduma za mikopo midogo midogo. Kadhalika, huduma za malipo ya ada mbali mbali kama vile ada za shule, kodi ndogo ndogo, faini ya makosa ya barabarani na malipo ya huduma kama za maji, umeme na televisheni. Benki kuu inaendelea kushirikiana na wadau wengine wa serikali ili kuahakikisha kuwa mifumo hii ya malipo pia inatumiwa katika kukusanya mapato ya serikali. 
Aidha, kuanzia Februari 2016, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza duniani kuweza kufanikisha malipo ya moja kwa moja kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine (wallet to wallet interoperability). Mafanikio haya yatawezesha wananchi kupata huduma za kifedha kwa mtandao kwa urahisi na unafuu zaidi.
Uboreshwaji wa huduma za malipo ya serikali kwa njia ya kieletroniki kama mbadala wa malipo kwa njia ya cheki za serikali, baada ya kuanzisha mfumo maalumu wa malipo ya serikali ambayo unasaidia sasa serikali kulipa mishahara, pensheni pamoja na mirathi bila kutumia cheki. Mfumo huu umesaidia kuleta uharaka na usalama katika malipo ya serikali na kupunguza mianya ya wizi uliokuwa unafanywa na wahalifu kutokana na mapungufu ya mfumo wa utoaji wa cheki za serikali. Aidha ili kusaidia malipo ya mishahara, Benki kuu pia iliongeza kiwango cha ukomo wa malipo kwa njia ya kutumiana kwenye akaunti za kibenki (Electronic Fund Transfer (EFT)) kutoka Milioni Kumi (10,000,000) ya awali hadi Milioni Ishirini (20,000,000/=) ili kuiwezesha serikali kulipa malipo mengi zaidi kwa njia hii.
 
Ili kuongeza matumizi ya malipo kwa njia ya kieletroniki katika halimashauri, Benki kuu iliamua kuunganisha halmashauri kwenye mfumo wa Malipo wa TISS (Tanzania Interbank Settlement System (TISS). Hadi sasa halmashauri zote katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza (isipokuwa Ilemela and Buchosa), Arusha, Mbeya (isipokuwa Busekelo), Dodoma (isipokuwa Kondoa and Chemba) na Songwe (isipokuwa Songwe and Tunduma) zimekwishaunganishwa, pamoja na hazina ndogo zote 24. Hali hii imesaidia kuongeza udhibiti wa malipo ya serikali pamoja na ufanisi katika ulipaji, hali ambayo imesaidia serikili kwa kiwango kikubwa kutekeleza malengo yake.
Katika juhudi za serikali kurahisisha na kuleta ufanisi katika ukusanyaji wa kodi na maduhuli mbali mbali, Benki Kuu imeendelea kufanikisha unganishwaji wa watoa huduma mbali mbali katika mifumo yake ya malipo. Kwenye mfumo wa TACH, Benki kuu imefanikiwa kuongeza Benki nne (4) tangu katika kipindi kifupi ambazo ni TIB Corporate Bank (December 2015), Tanzania Postal Bank (April 2016), Canara Bank Tanzania Ltd (September 2016) na Mwalimu Commercial Bank Plc (October 2016). Aidha, kwenye mfumo wa TISS, Benki Tatu (3) zaidi zimejiunga ambazo ni Canara Bank Tanzania Ltd , Meru Community Bank na  Mwalimu Commercial Bank Plc. Kujiunga kwa Benki hizi kwenye mifumo ya malipo ya Benki kuu, imeongeza wigo wa watoa huduma walio tayari kukusanya mapato ya serikali sehemu mbali mbali.
Ili kuunga mkono juhudi za serikali za kukusanya kodi na mapato mengine, Benki kuu imeongeza muda wa kuendesha mifumo yake ili kuwangezea walipaji muda zaidi wa kufanya malipo kupitia mifumo hii. Muda wa mfumo wa  TISS kufanya kazi umeongezwa kutoka saa 10 jioni hadi saa 2 za usiku. Aidha sasa hivi mfumo huu unafunguliwa pia siku za jumamosi na jumapili kinyume na hapo awali.
Benki kuu imeendelea kushirikiana na nchi nyingine za jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla ili kutengeneza na kuendeleza mifumo ya malipo inayovuka mipaka. Mfumo wa malipo wa Afrika Mashariki (East African Cross Border Payment System) umeendelea kuboreshwa ili uweze kutumiwa zaidi na wananchi wanaofanya malipo ndani ya nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika kipindi hiki, malipo yanayopita kwenye mfumo huu yamezidi kuongezeka, hususa ni yale yanayofanywa kati ya Tanzania na Kenya.
Mifuko ya Udhamini wa Mikopo
Benki Kuu, ambayo ni wakala wa Serikali kupitia Kurugenzi ya Masoko ya Fedha, husimamia Mifuko ya Udhamini wa Mikopo itolewayo na mabenki kwa sekta binafsi pamoja na sekta zinazojihusisha na uzalishaji na uuzaji wa mazao nje ya nchi. Kwa sasa Benki Kuu inasimamia mifuko miwili ambayo ni Mfuko wa Udhamini wa Mauzo Nje ya Nchi (ECGS) na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa kati (SME-CGS).
Katika kipindi cha Novemba 2015 mpaka Oktoba 2016 dhamana zenye thamani ya:
-          Shilingi 130,867,038,874.85 zilitolewa chini ya Mfuko wa Udhamini wa Mauzo Nje ya Nchi (ECGS). Kupitia mfuko huu, mabenki yameweza kukopesha vyama vikuu vya Ushirika na vya Msingi vinavyojishughulisha na ununuzi wa mazao na pembejeo za kilimo. Hali kadhalika; na
-          Shilingi 918,318,215 zilitolewa chini ya Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa kati (SME-CGS). Mikopo hiyo ilitolewa kwenye sekta za kilimo na ujenzi.
Huduma za Kibenki
Uharaka wa malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa serikali: Kwa karibu kipindi cha miezi 11 sasa tangu Novemba 2015, mishahara imekuwa ikilipwa kwa wakati na mara nyingi imekuwa ikilipwa kabla ya tarehe 25 ya mwezi husika ikilinganishwa na siku za nyuma.
Kuchelewa kulipa mishahara kumekuwa kukitokana na uhaba wa fedha hasa baada ya ukomo wa kukopa kufikia mwisho. Hii haikuwa mwenendo mzuri kwani wafanyakazi hawakuwa na uhakika wa siku ya kulipwa mshahara.
Kuongezeka kwa matawi ya Benki Kuu: Moja ya majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania ni kusambaza fedha katika matawi yake. Hadi June 2016, Benki Kuu ilikuwa na matawi matano, nayo ni; Mwanza, Arusha, Mbeya, Zanzibar na Dodoma.
Kwa vile Tanzania ina eneo kubwa; shughuli hii imekuwa na changamoto za usambazaji wa noti na sarafu katika maeneo ambayo Benki Kuu haina matawi yake. Ili kukabiliana na changamoto hii Benki Kuu imesaini mikataba na mabenki ya biashara ya usambazaji wa noti na sarafu kama ifuatavyo: -
(i)  Benki ya CRDB katika mikoa ya Mtwara, Kigoma, Sumbawanga, Songea na Tanga
(ii)  NMB katika mkoa wa Tabora
(iii) NBC katika mikoa ya Shinyanga na Bukoba
(iv)  PBZ katika kisiwa cha Pemba
Vituo hivi vyote vimekuwa vikifanya kazi kwa ufanisi; lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali; kubwa ikiwa ni udogo wa maghala yake kuhifadhi mahitaji halisi ya noti na sarafu kwa muda muafaka. Hali hii huilazimisha Benki Kuu kupeleka pesa mara kwa mara na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji.
Kutokana na changamoto hizi, Benki Kuu imejenga tawi jipya katika mkoa wa Mtwara ambalo limeanza kazi rasmi mefunguliwa tarehe 3 Octoba 2016. Benki Kuu inaamini kuwa tawi hili jipya litakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwenye eneo la kusini mwa Tanzania.
Miradi mikubwa ya viwanda na miundombinu inayoendelea na inayotarijiwa kuanza kazi siku za usoni itachangia katika kuimarisha uchumi.
  1. Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha  kisasa (Standard gauge)
  2. Ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda ambalo litahusu vile vile upanuzi wa bandari  ya Tanga
  3. Ujenzi wa Export Processing Zone ya Kurasini – itakayokuwa mhimili wa biashara kati ya China na Ukanda huu wa Afrika
  4. Mradi wa kuzalisha megawati 240 za umeme wa Kinyerezi II unaoendelea kujengwa.
  5. Miradi ya kupanua viwanja vya ndege nchini kwa mfano- Dodoma, na mingine inayoendelea -katika viwanja vya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya n.k.
  6. Ujenzi wa maghala ya taifa ya kuhifadhi chakula yenye uwezo wa kuhifadhi tani 350 yatakayojengwa kwa msaada wa Serikali ya Hungary katika sehemu mbalimbali nchini hususan katika mikoa inayozalisha mazao ya nafaka kwa wingi.
  7. Kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara ambacho kipo mbioni kuzalisha kulingana na uwezo wake (full capacity);
  8. Kiwanda cha kutengeneza marumaru cha Mkuranga, Pwani ambacho ujenzi wake unaendelea
  9. Kiwanda cha kuzalisha mbolea mkoani Lindi - kinajengwa
  10. Kiwanda cha bidhaa za chuma – mkoani Pwani ambacho kiko mbioni kukamilika.
Hitimisho
Maagizo mbali mbali yaliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano yamechochea ukuaji wa uchumi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Mwenendo wa viashiria mbalimbali vya shughuli za uchumi unadhihirisha kwamba hali ya uchumi wa Tanzania ni nzuri na inatoa matumaini makubwa. Matarajio ni kwamba endapo shughuli halali za kiuchumi zitaendelea kutekelezwa, lengo la ukuaji wa pato la Taifa la asilimia 7.2 kwa mwaka 2016 litafanikiwa. Hii inachangiwa pia na ukweli kwamba serikali ya awamu ya tano imejipanga katika kuimarisha uchumi endelevu usiokuwa na mianya ya rushwa; usimamizi thabiti wa rasilimali za umma; na ujenzi wa miundombinu bora kwa lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

No comments:

Post a Comment