Friday, 7 October 2016

Hivi ndivyo Rais Magufuli alivyozindua Kiwanda cha kwanza cha Azam Fruits Processing Plant, Mkuranga Pwani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 
Oktoba, 2016 amezindua kiwanda cha 
kusindika matunda kinachomilikiwa na 
kampuni za kitanzania za Bakhresa katika 
eneo la Mwandege, Wilaya ya Mkuranga 
Mkoani Pwani.


Kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda 13
vinavyomilikiwa na kampuni za Bakhresa 
vilivyopo Dar es Salaam na Pwani, kina 
uwezo wa kusindika tani 350 za matunda 
kwa siku, kimeajiri karibu wafanyakazi 1,000
 na uwekezaji wake umegharimu takribani 
Shilingi Bilioni 261.

Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda 
hicho cha kwanza tangu aingie madarakani
 Rais Magufuli amempongeza Mwenyekiti 
wa kampuni za Bakhresa Bw. Said Salim 
Bakhresa kwa uwekezaji huo na amesema 
Serikali yake itamuunga mkono yeye na 
wawekezaji wengine ambao wanazalisha 
ajira na kulipa kodi ipasavyo.

"Nawapenda wafanyabiashara wanaolipa 
kodi, nawachukia wafanyabiashara ambao 
hawalipi kodi, nawapenda wafanyabiashara 
wanaotengeneza ajira kwa watanzania, 
wewe umetengeneza ajira za watanzania, 
na umeendelea kutengeneza ajira kule mjini 
kwa wauza juisi na wengine, lakini pia 
unatengeneza ajira kwa wakulima.



Mtu akitengeneza nanasi zake anajua kuna 
soko la kupeleka, mtu akilima maembe yake 
anajua kuna soko la kupeleka" amesema 
Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli ametoa miezi miwili kwa 
Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania 
(TANESCO) kupeleka umeme katika 
kiwanda hicho ili kupunguza gharama za 
uzalishaji zinazosababishwa na kutumia 
umeme unaozalishwa na majenereta.

Pia ameahidi kuzifanyia kazi changamoto 
zilizotajwa na mmoja wa Wakurugenzi wa 
kampuni za Bakhresa Bw. Abubakar Said 
Salim Bakhresa zikiwemo kupatiwa gesi 
asilia kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya 
kusindika matunda na urasimu 
unaosababishwa na wingi wa taasisi 
zinazodhibiti uzalishaji wa bidhaa.

Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa
 kampuni za Bakhresa kuwekeza katika 
uzalishaji wa sukari ili kukabiliana na tatizo 
la uhaba wa bidhaa hiyo na amesema 
endapo kampuni hiyo ipo tayari Serikali 
itatoa eneo la kuzalisha miwa na kujenga 
kiwanda.

Mapema akitoa taarifa juu ya hali ya 
viwanda katika mkoa wa Pwani, Mkuu wa 
Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo 
amesema pamoja na viwanda viwili vya 
kampuni za Bakhresa vilivyopo Mkoani 
Pwani, Mkoa huo unavyo viwanda vingine 
88 ambavyo vinazalisha bidhaa na vingine 
vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, 
vikiwemo viwanda viwili vikubwa Afrika 
Mashariki na Kati ambavyo ni kiwanda cha 
uzalishaji wa vigae (Tiles) na kiwanda cha 
kuzalisha nondo na vyuma vya madaraja 
vitakavyokamilika ifika Desemba mwaka 
huu.

Vingozi wengine waliohudhuria uzinduzi huo
ni Waziri wa Viwanda, Biashara na 
Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Mbunge 
wa Mkuranga Mhe. Abdallah Ulega na 
Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na 
Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru.

Waziri wa viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage (kushoto) na katibu Mkuu wake Dkt. Adelhelm Meru wakiongea na Mwenyekiti wa makampuni ya Bakhresa Group Mzee Said Salim Bakhresa wakati wakimsubiri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwasili kwenye sherehe za ufunguzi wa kiwanda cha kusindika matunda cha Bakhresa Food Products kijijini Mwandege wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani  Oktoba 6, 2016

Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kundi la Makampuni ya Bakhresa Hussein Sufian Ally kuhusiana na hatua mbalimbali za usindikaji wa matunda katika kiwanda hicho kilichopo Mwandege mkoani Pwani.


 USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment