Friday, 28 October 2016

Ripoti ya Mkataba wa Lugumi yafikishwa mikokoni Spika wa Bunge.

Image result for Job Ndugai.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Projestus Rwegasira amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge ya kuhakikisha mfumo wa vifaa vya utambuzi wa alama za vidole unafungwa katika wilaya za kipolisi 108 nchi nzima kwa muda wa miezi mitatu.

Zabuni ya kufunga na kusambaza mashine hizo za utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi ulifanywa na Kampuni ya Lugumi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo Naghenjwa Kaboyoka, aliwathibitishia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa ripoti hiyo tayari imekabidhiwa kwa Ofisi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Kaboyoka alisema ripoti hiyo baada ya kukabidhiwa kwa Spika Ndugai ataipitia na baadaye kuiwasilisha kwa kamati hiyo ya PAC.

Juni 30, mwaka huu, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya kuahirisha Bunge la Bajeti aliiagiza serikali kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi kwa ajili ya kuwadhibiti wahalifu na kuitaka Kamati ya PAC ifuatilie suala hilo.

Dk Tulia alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa yenye utata ya kuhusu zabuni yenye thamani ya Sh bilioni 37 ya kufunga mashine hizo katika vituo vyote vya Polisi baina ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited iliyotolewa mwaka 2011.

“Ninashauri serikali ihakikishe mradi huu unakamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia leo…, mradi huu utasaidia Jeshi la Polisi kuwatambua kwa haraka watu waliohusika katika matukio ya uhalifu mbalimbali,” alisema.

Katika mkataba huo, Lugumi inatakiwa kusambaza na kufunga mashine hizo za utambuzi wa vidole katika wilaya 108 za kipolisi nchi nzima.

Hata hivyo, mashine hizo zilifungwa kwenye vituo 14 pekee wakati tayari kampuni hiyo ilishapokea kiasi cha asilimia 99 za malipo yake.

Katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2013/14 ilionesha kuwa pamoja na kampuni hiyo ya Lugumi kulipwa asilimia 99 ya malipo sawa na Sh bilioni 34, bado haijakamilisha mradi huo kwa muda wa miaka mitano sasa.

Aprili, mwaka huu, PAC iliunda kamati ndogo kwa ajili ya kuchunguza mkataba huo wa utata baina ya Kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi.

No comments:

Post a Comment