Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza kufuatia kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mafinga Mkoani Iringa na Waziri Mstaafu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Joseph Mungai.
Mhe. Joseph Mungai ambaye alishika nyadhifa mbalimbali za uongozi Serikali ikiwemo Uwaziri katika Wizara mbalimbali amefariki dunia leo tarehe 08 Novemba, 2016 Majira ya Jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha Mhe. Joseph Mungai ambaye alimfahamu kama mchakapakazi, mtu aliyesimamia alichokiamini, mpenda maendeleo na aliyependa kufanya kazi kwa ushirikiano.
“Nilifanya kazi na Mhe. Mungai ambaye wakati akiwa Waziri wa Elimu na Ufundi, mimi nilikuwa Waziri wa Ujenzi, tulikuwa tukishirikiana na kushauriana kwa mambo mengi yenye manufaa kwa Taifa.
Nimesikitishwa sana na kifo chake na namuomba Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza anifikishie salamu zangu za pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Mufindi na wabunge wote Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amemuombea Marehemu Joseph Mungai apumzishwe mahali pema peponi. Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Novemba, 2016
USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE
No comments:
Post a Comment