Tuesday 29 November 2016

Wizara ya Elimu yatoa ufafanuzi kuhusu wanafunzi wa Diploma kujiunga vyuo vikuu.

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa ufafanuzi kwamba haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa kujiunga na vyuo vikuu badala yake walichokataza ni wanafunzi waliofeli kidato cha nne na cha sita kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti vyenye sifa.

Aidha, imesema kwa waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni wajibu wa waajiri wao kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na kutumia fursa hiyo kufanya mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo jana Dar es Salaam kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea mitandaoni kwamba serikali imepiga marufuku watu wenye Stashahada kujiunga na vyuo vikuu badala yake watakaoingia ni wenye sifa za kidato cha sita.

Manyanya alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na sifa za shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya kufanya mitihani hiyo waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kusoma vyuo vikuu.

“Ni vitu tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu anakaa nafasi kwa sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki utafanyika kwa vyeti na wanaofanya hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu Waziri.

Alisema kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo zilikuwa hazitakiwi kwa wakati huo ni batili zitafutwa na kwa watakaoingia kwa sasa vyuoni kwa kutumia njia zisizo rasmi na kubainika hata ikifika mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa taarifa tayari wanayo.

“Kilichoongelewa siku ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha sita waliofeli kuingia kwenye ‘foundation course’ na diploma haikutajwa pale kwa kuwa haikuulizwa na hakuna kauli iliyotajwa pale kukataza watu wa diploma kwenda chuo kikuu,” alieleza Manyanya akirejea kauli ya Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni katika mahafali ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.

Profesa Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.

“Nami ningependa nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei mtu sifa. Kama sifa ya kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha sita, kama amefeli Baraza la Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa nini anakwepa kule? Kwa nini? Kwa nini tunataka tuendeleze uchochoro,” alieleza Waziri Ndalichako.

Naibu Waziri alisema kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo njia ya moja kwa moja na njia ya mbadala ya kuwa na vyeti vinavyotambulika na kinasimamiwa na mamlaka husika ambayo ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na wawe na ufaulu mzuri.

“Tanzania imejiwekea mifumo yake ya elimu ambayo inaendana na ngazi za kimataifa katika utoaji wa elimu na hapo awali tulikusudia kuhakikisha elimu inatolewa kwa watu wengi zaidi na hizo fursa zinawafikia wadau wote katika ngazi mbalimbali kwa kupanua elimu ya msingi hadi vyuo vikuu,” alieleza Naibu Waziri.


USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE



                                SUBSCRIBE ON YOUTUBE 
                                          
                                               TIKISA TV

1 comment: