Baada ya kuwa nje ya uwanja kwa takriban mwezi mzima, straika wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma, amerejea kwenye kikosi hicho na yupo fiti kucheza mbele ya Waarabu MC Alger ya Algeria kwenye mechi ya Kombe la Afrika.
Ngoma amekuwa akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara tangu ulipoanza mzunguko wa lala salama wa Ligi Kuu Bara, kiasi cha kumfanya ashindwe kuitumikia Yanga kwenye michezo muhimu mbalimbali iliyokuwa mbele yao ukiwemo ule dhidi ya Simba ambao walifungwa mabao 2-1.
Daktari wa Yanga, Edward Bavu, alisema Ngoma ana asilimia 100 za kucheza mchezo huo kwani yuko fiti na kwamba ana zaidi ya wiki mbili tangu apone ambapo alikuwa akifanya mazoezi na timu.
“Sina shaka tena na hali ya Ngoma ambaye alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mguu, tayari amesharejea uwanjani na kwamba ana uhakika wa kucheza dhidi ya MC Alger Jumamosi (kesho), hali yake kwa jumla inaridhisha sana na kwamba amepata muda mrefu wa kufanya mazoezi na wenzake.
“Mashaka yapo kwa Amissi Tambwe, kwani yeye alianza mazoezi jana (juzi), hivyo siwezi kumpa asilimia nyingi za utimamu wa mwili wake kwani mazoezi yake hayakidhi sana, hivyo kucheza kwake itategemeana na mahitaji ya mwalimu na namna yeye atakavyomuona kwenye mazoezi haya ya siku mbili zilizosalia.
“Ukiachana na hao, kuna Thabani Kamusoko na Justine Zulu, hawa hali zao bado haziko vizuri kwani hata mazoezi hawajaanza na Kamusoko aliumia siku moja kabla ya mchezo wetu na Azam, huku Zulu yeye akishonwa nyuzi sita baada ya kuumia kwenye mchezo huo,” alisema Bavu.
No comments:
Post a Comment