Wednesday, 24 May 2017

Maagizo aliyoyatoa Rais Magufuli baada ya kuvunja bodi TMAA

Related image
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na pia kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wake kwa kushindwa kusimamia vyema sekta ya madini.

Mbali na kuchukua hatua hiyo, Rais Magufuli ameviagiza vyombo husika pia kuwachukulia hatua watendaji wa TMAA na Wizara ya Nishati na Madini waliohusika kuisababishia hasara serikali kutokana na mchanga wa madini uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akipokea taarifa kuhusu ripoti ya ukaguzi wa mchanga wa madini wa makontena 277 yaliyozuiliwa bandarini.

“Bodi ya TMAA nimeivunja kuanzia leo. Mkurugenzi Mtendaji wa TMAA anasimama kazi kuanzia leo lakini vyombo vya dola ambavyo vipo hapa muanze kuwafuatailia wafanyakazi wa TMAA waliohusika na mlolongo wote ili hatua za kisheria zianze kuchukuliwa” alisema Rais Dkt Magufuli.

Lakini wakati huo huo Rais Magufuli ameikosoa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushindwa kuisimamia vizuri TMAA ambayo ipo chini yake, na hivyo kuisababishia serikali hasara kubwa kutokana na usafirishwaji wa mchanga nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment