Kampuni ya SportPesa imesema mechi ya kirafiki kati ya Everton ya England dhidi ya Gor Mahia ya Kenya itaitangaza Tanzania kimataifa zaidi.
Everton itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia Julai 13 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Gor Mahia ndiyo mabingwa wa SportPesa Super Cup.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Everton, Pavel Slavkov amesema ana imani kubwa Tanzania itasikika sana katika kipindi ambacho Everton itakuwa nchini.
Akizungumza na Mtanzania, Slavkov amesema inakuwa ni mara ya kwanza timu ya inayoshiriki Ligi Kuu England kufanya ziara katika nchi za Afrika Mashariki tena katika kipindi ambacho inajiandaa na ligi kuu.
“Si kipindi cha utani, ni kipindi cha maandalizi ya Premier League. Unawaona Everton wanakuja Tanzania. Wapenda soka wengi watageuza macho na masikio yao hapa Tanzania kwa ajili ya Everton.
“Hii itafanya wengi waanze kujua kuhusiana na Tanzania hasa kimichezo lakini pia inawezekana suala la kutaka kutembelea na kadhalika. Hivyo ni vizuri wapenda mpira na wapenda michezo tuungane kuwakaribisha wageni wetu na kuwaonyesha ukaribu na kuwa Tanzania ni nchi salama na yenye amani,” alisema.
No comments:
Post a Comment