Maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Gor Mahia ya Kenya na Everton ya England, utakaofanyika Julai 13, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, yamekamilika.
Tayari Gor Mahia kutoka Kenya - Mabingwa wa SportPesa Super Six, imetua hapa Dar es Salaam, Tanzania leo Jumanne, Julai 11, mwaka huu tayari kabisa kwa mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 11.00 jioni.
Kwa upande wa Everton, wao wameingia alfajili Julai 12, mwaka huu tayari kabisa kuwakabili Gor Mahia katika mchezo ambao tayari tumetangaza kuwa Kiingilio kitakuwa ni Sh 3,000 kwa mzunguko na Sh 8,000 kwa majukwaa ya watu maalum.
Timu zote zitahudumiwa sawa kuanzia usafiri, hoteli na huduma za tiba hapa uwanjani kuanzia siku ya mazoezi na siku ya mchezo wenyewe. Kila timu itapata dakika 45 mazoezi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Gor Mahia watacheza Jumanne katika uwanja huu wa Taifa na Everton - zamu yao itakuwa leo Jumatano. Tumeweka muda huo kutokana na ushauri wa wataalamu wa waliofanya marekebisho ya uwanja na namna bora wa kutunza uwanja.
Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunatarajia atakuwa mgeni rasmi kwenye mchezo huo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yussuf Singo amethibitisha hilo.
Kuhusu viingilio, Ndugu zetu wa Selcom, tumekuwa nao pamoja na leo wanatuthibitishia kuwa wamekwisha kuanza kuuza tiketi katika mtandao.
Ikumbukwe tu tumeweka viingilio vya bei nafuu ili kuwapa Watanzania wengi fursa ya kuingia uwanjani kushuhudia mechi hiyo ambayo timu zote ngeni, lakini kwa kuwa Watanzania ni watu wa mpira, bila shaka watapata burudani murua na maridhawa kabisa siku ya Alhamisi.
Ulinzi umewekwa wa kutosha kabisa kwani kutakuwa na mbwa, farasi, magari ya kumwaga maji yenye kuwasha mwili kwa wale ambao watabainika kuleta vurugu.
Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama yakiwamo makampuni ya binafsi ya ulinzi, wametuhakikishia kwamba watadhibiti kila aina ya vurugu zitakazotokana na mashabiki wakorofi ambao wao huwaza vurugu kwa sababu zao mbalimbali.
Mchezo utaanza saa 11.00 jioni na utarushwa hewani na vyombo mbalimbali vya habari vya ndani kwa maana ya ninyi wenzetu kadhalika vya nje ya mipaka ya Tanzania.
TFF wametuambia kwamba wameratibu vema kabisa mchezo huo katika maeneo ya Itifaki, ufundi na vyombo vya habari.
Kuhusu ufundi uwanjani ni kwamba Mwamuzi wa mchezo huo atakuwa Israel Mujuni Nkongo wa Dar es Salaam, ambaye atakuwa mwamuzi wa kati; akisaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza - mshika kibendera wa kwanza na Frank Komba ambaye atakuwa mshika kibendera wa Pili.
Mwamuzi wa akiba atakuwa ni Elly Sasii. Waamuzi wote hao ni wale wa beji za FIFA. Kamisha wa mchezo huo atakuwa ni Michael Richard Wambura wa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment