Tuesday, 29 August 2017

Hali halisi aliyoikuta TAKUKURU Rais Magufuli baada ya kutembelea atoa Maagizo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutokuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua pale wanapokuwa na ushahidi dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo  tarehe 28 Agosti, 2017 alipotembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa TAKUKURU katika ofisi za makao makuu ya taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.

“Kuna mambo mengi ya hovyo yanafanyika, tumehakiki pembejeo za ruzuku na kubaini madai ya Shilingi Bilioni 48 ni hewa, tumebaini wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500, tumebaini kaya masikini hewa 56,000 zilizopaswa kupata fedha TASAF, tumebaini wanafunzi hewa 5,850 waliotakiwa kupata mkopo, kuna vichwa vya treni 11 vimeletwa bila kuwepo mkataba na mengine mengi, haya yote yanafanyika kwa rushwa, nataka kuwaona mnachukua hatua stahiki” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amesema ana imani na TAKUKURU na amewataka wafanyakazi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uzalendo na uadilifu mkubwa na kwamba Serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili.

Katika mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amepokea masuala mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi wa TAKUKURU na amewaahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi ili kuboresha maslahi yao na mazingira ya kazi.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Katibu Mkuu Dkt. Laurian Ndumbaro na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Valentino Mlowola.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi na wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge Hydropower Project), ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa barabara mbalimbali nchini, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika Mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Matogolo Kalemani ametoa taarifa ya maandalizi ya awali ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’ Gorge na kwamba zabuni ya kuanza kwa ujenzi huo itatangazwa tarehe 30 Agosti, 2017.
Mhe. Rais Magufuli amesema fedha za kuanza kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa utakaozalisha Megawatts 2,100 zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa zipo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

28 Agosti, 2017

No comments:

Post a Comment