Golikipa wa Singida United Peter Manyika Jr ameendelea kuonyesha kiwango bora baada ya kucheza mechi saba bila kuruhusu nyavu zake kuguswa akiwa na klabu yake hiyo ambayo imepanda daraja msimu huu.
Mechi ya jana ambayo Singida United walishinda bao 1-0 dhidi ya Lipuli FC, imemfanya Manyika kufikisha jumla ya michezo saba bila kufungwa katika mechi 10 za VPL alizocheza msimu huu wa 2017/18.
Mtoto huyo wa golikipa wa zamani wa Yanga Peter Mantika sasa amefikia rekodi ya golikipa wa Azam Razak Abarola ambaye hajaruhusu goli katika mechi saba za VPL katika mechi tisa alizochezan hadi sasa msimu huu.
Golikipa mwingine ambaye amecheza mechi nyingi bila kuruhusu goli ni Aishi Manula ambaye ni golikipa namba moja wa klabu ya Simba na Taifa Stars, hajaruhusu goli katika mechi tano za VPL kati ya mechi tisa alizocheza hadi sasa.
Manyika tayari amecheza michezo 10 wakati Manula akiwa na mechi tisa huku leo akitarajiwa kucheza mechi yake ya 10 ambayo klabu yake ya Simba itacheza na Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.
Manyika amejiunga na Singida United msimu huu akitokea Simba ambako alikosa nafasi ya kuchcza mara kwa mara lakini tangu ametua kwenye kikosi hicho cha kocha Hans Van Pluijm amejihakikishia nafasi ya kuanza.
No comments:
Post a Comment