KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre, tayari ameshakipanga kikosi chake ambacho kitaanza leo Jumatano kwenye mchezo wao dhidi ya Al Masry ya Misri, huku akiwapa jukumu zito la kufunga mabao washambuliaji wake, Emmanuel Okwi na John Bocco.
Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa ni wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika na utaanza majira ya saa 12 jioni, ingawa Lechantre hakufurahishwa na muda huo uliopangwa na viongozi.
Katika mazoezi ya juzi Jumatatu yaliyoanza majira ya saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Boko uliopo jijini Dar, Championi lilimshuhudia Lechantre akipanga kikosi chake kilichoonekana ndicho cha maangamizi ambacho kitatumika kummaliza Mwarabu leo.
Katika kikosi hicho ambacho golini yupo Aishi Manula, walinzi wake ni Shomary Kapombe, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Yusuf Mlipili na James Kotei.
Kwenye kiungo wapo;
Jonas Mkude
Nicholaus Gyan
Shiza Kichuya
Bocco na Okwi.
Katika mazoezi hayo yaliyomalizika saa 1:30 usiku, kocha huyo alikuwa makini zaidi kwenye kushambulia kupitia pembeni.
Aliwapa wachezaji wake haswa wa pembeni namna ya kushambulia kwa kasi na kupiga krosi za maana ikiwemo kupiga pasi za mipira mirefu huku akiwaeleza kuwa mara nyingi Waarabu hawana kasi lakini wana uhakika na wanachokifanya.
Akiwazungumzia wapinzani wao hao, Lechantre alisema:
“Tunakwenda kukutana na moja kati ya timu bora Afrika ambayo inashiriki ligi bora, timu za Misri ni imara, kikweli Al Masry ni timu nzuri na tunaiheshimu.” “Sitabadilisha mfumo, nitakuwa na washambuliaji wangu wawili, Bocco na Okwi, kwenye kiungo tutaangalia itakavyokuwa pengine nitakuja na ‘sapraizi’ baab kubwa, njooni mkaone.”
Makipa wafanya mazoezi kwa saa matatu
Katika hali ambayo haikutarajiwa, kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo ya jumla, Championi liliwashuhudia makipa wanne wa kikosi hicho wakianza mazoezi mapema tu kuanzia saa 10:30 jioni wakisimamiwa na kocha wao, Muharami Mohammed.
Makipa hao ni Aishi Manula, Said Mohammed ‘Nduda’, Emmanuel Mseja na Ally Salim, walipoanza muda huo, walikuja kumaliza saa 1:30 sawa na wenzao. ambapo jumla walifanya mazoezi kwa muda wa saa tatu tofauti na siku zote.
No comments:
Post a Comment