Baada ya Yanga kuanza vibaya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera raia wa DR Congo, amesema kuwa ni lazima washinde mechi yao ijayo dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda.
Yanga ilianza hatua hiyo kwa kufungwa mabao 4-0 na USM Alger ya Algeria ambapo keshokutwa Jumatano itacheza na Rayon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Katika michuano hiyo, Yanga imepangwa Kundi D pamoja na USM Alger ya Algeria, Rayon Sport (Rwanda) na Gor Mahia kutoka Kenya.
Kwa mujibu wa gazeti la Championi, Zahera alisema: “Hatukuweza kufanya vizuri kwenye mchezo wa kwanza kutokana na kutokuwa na kikosi kamili kwa sababu wengine waligoma, nadhani mnajua, na mmesikia hilo.
“Lakini hivi sasa tunajipanga kwa mchezo ujao kuhakikisha tunashinda, tangu nimekuja hapa nimekuwa nikiwafuatilia wapinzani wetu tuliokuwa nao kundi moja, lakini kilichokuwa kinanifanya nisiweze kufanikiwa kuwaandaa vizuri wachezaji ni kutokana na wengine kukosekana.
“Hivi sasa wachezaji wangu wapo vizuri na matumaini yangu ni kuona tunafanya vizuri tukianza na mchezo huo dhidi ya Rayon hapa nyumbani.”
No comments:
Post a Comment