UPO
uwezekano mkubwa wa mastaa wakubwa Simba kutimka kwenye klabu hiyo
kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara baada ya kupata ofa nono za kucheza
soka nje ya nchi, ikiwemo Afrika Kusini.
Mastaa
hao wanaotaka kuondoka Simba wote mikataba yao inatarajiwa kumalizika
mwishoni mwa msimu huu ambao ni Sharraf Eldin Shiboub na Hassani Dilunga
huku mmoja Clatous Chama akiwa na mkataba wa mwaka mmoja.
Kati
ya wachezaji hao, wapo wale ambao tayari uongozi wa Simba umeanza
mazungumzo nao kwa ajili ya kuwaongezea mikataba ya kuendelea kukipiga
Simba kwenye msimu ujao.
Habari
zinaeleza Chama anahitajika na moja na klabu kubwa Afrika Kusini ambayo
ipo kwenye mazungumzo huku Yanga ikitajwa nayo kuwania saini yake.
Mtoa
taarifa huyo alisema kuwa Dilunga anahitajika na nchi za Afrika Kusini
na Uarabuni na huenda akatimka mara baada ya maambukizi ya Virusi vya
Corona kumalizika.
Aliongeza
kuwa na Shiboub anahitajika na klabu kubwa za Afrika Kusini, Sudan na
Misri ambazo zote zimeonyesha nia ya kumhitaji na yeye mwenyewe ameomba
aondoke kwa kile kinachodaiwa kutokuwa na mahusiano mazuri na kocha
mpya, Mbelgiji Sven Vandenbroeck.
“Simba
huenda ikapata pigo kubwa la kuondokewa na viungo wake watatu wakubwa
katika msimu ujao wa ligi, ni baada ya wachezaji wenyewe kuonekana
kutaka kuondoka.
“Kati
ya wachezaji hao wanaotaka kuondoka, wawili wameonekana kutokuwa na
furaha na timu hiyo kwa kile kilichoelezwa kutokuwa na mahusiano mazuri
na kocha.
“Wachezaji
hao walifuatwa na viongozi kwa ajili ya kuongeza mikataba mipya lakini
wameomba mazungumzo yafanyike mara baada ya mikataba yao kumalizika,”
alisema mtoa taarifa huyo.
Aidha,
Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Senzo Mazingisa hivi karibuni alisema
kuwa timu yao haitakubali kumuachia mchezaji yeyote watakayemuhitaji
ambaye mkataba wake unamalizika na badala yake itapambana kumbakisha.
No comments:
Post a Comment