UONGOZI wa Klabu ya Simba umeibuka na kutoa msimamo wao juu ya nini kitaendelea kwao endapo itatokea serikali na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) wakaamua kufuta msimu huu wa 2019/20 wa Ligi Kuu Bara kutokana na janga la Virusi vya Corona.
Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara amesema kuwa wao hawana tatizo kama itatokea ligi ikifutwa, kwa kuwa bado watakuwa wanayo nafasi ya kwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kwa kuwa wao ni vinara na wana nafasi ya kuwa mabingwa wa nchi.
Mijadala ambayo inaendelea hivi sasa miongoni mwa wadau wa soka nchini ni kuhusiana na mustakabali wa ligi zote Tanzania huku baadhi ya wapenda soka wakiwemo wabunge wakishauri ligi ifutwe na Simba wapewe ubingwa.
Akizungumzia msimamo wao, kama klabu Manara alisema: “Kama ligi ikifutwa, hatuna shida sisi kama Simba, kwa sababu kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa tunajua hiyo ni nafasi yetu sisi na siyo timu nyingine.
“Kwa sababu ligi ikifutwa bado Simba atakuwa kileleni, ikiendelea bado Simba watakuwa mabingwa hilo halina mjadala, kwa hiyo kwa lolote litakalotokea, timu yetu ndiyo itaiwakilisha nchi kimataifa na siyo Yanga wala Coastal Union.
“Hao Fifa kama wakisema ligi zote zifutwe, lazima watayataka mashirikisho kuchagua wawakilishi wao wa mashindano ya kimataifa na kigezo kitakuwa kuchukua timu mbili zinazoongoza msimamo, kwa hiyo hao wanaoshangilia ligi kufutwa pole yao,” alsema Manara.
No comments:
Post a Comment