Rais wa Afrika
Kusini Jacob Zuma ameahidi kuwa vyuo vikuu havitaongeza ada ya masomo
mwaka ujao baada ya wanafunzi wa vyuo hivyo kuandamana kwa wiki moja.
Maandamano hayo ya wanafunzi ndiyo makubwa zaidi kushuhudiwa nchini humo tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi 1994.Wanafunzi hao awali walikataa pendekezo la serikali la kuweka nyongeza ya ada katika 6%, badala ya kati ya 10% na 12% iliyokuwa imependekezwa na wasimamizi wa vyuo.
Bw Zuma alitangaza hatua hiyo huku mamia ya wanafunzi wakikusanyika nje ya afisi yake.
Kabla yake kuhutubu kupitia runinga, polisi walikuwa wametumia mabomu ya kutawanya waandamanaji kutawanya wanafunzi waliotaka kuingia jengo la Union Building, lenye makao makuu ya serikali mjini Pretoria.
Jumatano, polisi walikuwa wamekabiliana na wanafunzi waliokuwa wakitaka kuingia majengo ya Bunge mjini Cape Town.
Vyuo vikuu kadha tayari vilikuwa vimefungwa kutokana na machafuko hayo.
"Tumekubaliana kwamba karo ya vyuo vikuu haitaongezwa mwaka 2016,” Bw Zuma alisema baada ya kukutana na wakuu wa vyuo na wawakilishi wa wanafunzi.
“Kuna mambo ambayo yamebuliwa mkutanoni ambayo yanahitaji kufuatiliwa zaidi – haya ni pamoja na elimu bila malipo, vyuo kujisimamia na ubaguzi wa rangi.”
No comments:
Post a Comment