Tuesday 3 November 2015

Kafulila asema haya kuhusu Jimbo lake


                                 David Kafulila
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila, ambaye ametangazwa kushindwa katika jimbo hilo uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, ameibuka na kusema anakusudia kwenda mahakamani ili atangazwe kuwa mshindi wa jimbo hilo.
Amedai kwa mujibu wa kura alizokusanya kupitia mawakala wake katika vituo 182, alishinda kwa kura 34,149 dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Husna Mwilima, aliyepata kura 32,982, lakini tume ikamtangaza kuwa mshindi.
Kafulila alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uchaguzi huo, akidai ameporwa ushindi wake na nguvu ya dola imetumika kuhakikisha anakosa ushindi huo.
“Ninachofahamu mimi ni Mbunge wa Kigoma Kusini, ila nilihujumiwa na watumishi wa tume kwa kubadili matokeo yangu na kumtangaza mgombea wa CCM kuwa ni mshindi, hivyo nitaenda Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kudai haki yangu na kutangazwa mshindi,” alisema Kafulila.
Alisema atakachokifuata mahakamani siyo kurudiwa kwa uchaguzi bali kuiomba mahakama kumtangaza mshindi kwani ana vielelezo vyote.
“Wiki ijayo nitakuwa nimekamilisha mipango ya kwenda mahakamani, nina fomu zote 382 kutoka katika kila kata, vituo 182 vilivyotumika kupiga kura zinazoonyesha idadi ya kura zangu. Nina imani mahakama haitatumia mlolongo mrefu kutoa hukumu kwa sababu nina vielelezo vya kutosha,” alisema Kafulila.
Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutokata tamaa na taarifa za kukosa ubunge wake na kuwataka kuwa wavumilivu wakati wakisubiri maamuzi ya mahakama.
KASHFA YA ESCROW
Kafulila alipoulizwa sababu anayodhani kumkosesha jimbo hilo au kuibiwa ushindi kama alivyodai, alisema kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Bunge lililopita ya kuibua masuala ya ufisadi ikiwamo sakata la Tegeta Escrow.
Alidai kudhibitisha kuwa njama zilitumika,  aliwekewa ulinzi mkali wa dola wakati wa upigaji kura na kipindi cha kusubiri matokeo.
“Nguvu ya dola ilitumika sana ili kuhakikisha Kafulila ninashindwa, polisi walikuwa ni wengi sana pia matokeo yalichelewa kutangazwa isivyo kawaida,” alisema.
 Kafulila alisema alishangazwa na kitendo cha mawakala wa tume kuahirisha kazi ya ujumuishaji wa kura mara kwa mara licha ya sheria ya uchaguzi kutoruhusu.
“Kazi ya ujumuishaji ilikuwa ikiahirishwa mara mbili na wakati mwingine kuchukua zaidi ya saa 7 na saa 10 hali ambayo siyo ya kawaida,” alidai Kafulila.
Akizungumzia hatma yake juu ya kupiga vita ufisadi,  Kafulila alisema ataendelea na harakati hizo.
Alisema kwa sasa anaandaa vitabu vinavyozungumzia ufisadi kikiwamo kinachoitwa ‘Escrow Unfinished Business’, ambacho kinaelezea vizuri masuala hayo ambayo amekuwa akiyapiga vita.
Uchaguzi mkuu ulifanyika Oktoba 25, mwaka huu, katika Jimbo la Kigoma Kusini, Mwilima wa CCM alitangazwa mshindi kwa kupata kura 34,453, dhidi ya Kafulila aliyepata kura 33,382.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment