Tuesday 3 November 2015

Raisi Kikwete asema yakwake kuhusu mzozo wa Uraisi Zanzibar



              Raisi wa Jakaya Kikwete 

RAIS Jakaya Kikwete ameeleza kuguswa kwake na hali ya kisiasa na usalama wa Zanzibar na kusema anafanya juu chini kuhakikisha suluhu inapatikana kwa amani, huku Ikulu ikikanusha kupokea maombi kutoka kwa Mgombea Urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad akitaka kukutana na Rais Kikwete.
Seif anadai kupeleka maombi hayo kwa Rais Kikwete baada ya uchaguzi wa Zanzibar kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
“Ikulu inapenda kukanusha kwamba ilipokea maombi kutoka kwa Mheshimiwa Hamad ya kukutana na Rais Kikwete …” ilisema sehemu ya taarifa ya Ikulu, iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba alichopokea Rais Kikwete, ilikuwa ni malalamiko ya CUF kuhusu vitendo kadhaa vya Jeshi la Polisi Zanzibar. Pia ilieleza kuwa Rais Kikwete aliombwa na CUF kuwezesha mazungumzo kati ya Hamad na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange.
Wakati huo huo taarifa hiyo ya Ikulu imesema kwamba Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, amemwamuru Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu kufanya uchunguzi wa madai hayo ya CUF na kutoa taarifa kwake.




                Mgombea wa Urais Zanzibar Sharif Hamad 

Aidha, ameamuru ofisi yake kuwezesha mazungumzo kati ya Jenerali Mwamunyange na maofisa wa CUF.
“Ikulu inapenda kuthibitisha kwamba Rais Kikwete, kama ilivyo kwa Mtanzania yeyote, anaguswa na hali ya siasa na usalama wa Zanzibar, na amekuwa akifanya juu chini na kushauriana kwa mapana katika siku chache zilizopita, kutafuta suluhisho la amani katika Zanzibar,” ilisema taarifa hiyo.
Wakati suala hilo likiendelea kubaki mikononi mwa chombo huru cha uchaguzi visiwani Zanzibar, Rais Kikwete amesema yuko tayari kufanya kila liwezekanalo, kuhakikisha hali inakuwa kawaida visiwani humo.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema haitavumilia aina yoyote ya vurugu visiwani humo wakati ikisuburi Uchaguzi Mkuu baada ya uliofanyika Oktoba 25 kufutwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, alisema hayo jana katika taarifa aliyotoa kwa vyombo vya habari.
“Kila mmoja lazima aendelee na maisha yake kama kawaida wakati tukisubiri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutoa ratiba kwa ajili ya uchaguzi mpya. ZEC ni chombo huru na hakuna mtu yeyote au taasisi inayoweza kuingilia kazi zake. Ilifuta uchaguzi na tunapaswa kuheshimu uamuzi wake,” alisema Aboud.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa huku Chama cha Wananchi (CUF) kikipinga kufanyika uchaguzi upya kwa madai kwamba uchaguzi uliofutwa, ulikuwa huru na haki kama ambavyo waangalizi wa ndani, ikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) walivyobaini.
Mgombea Urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad anashinikiza Mwenyekiti wa NEC, Jecha Salim Jecha aendelee kutangaza haraka matokeo na mshindi, kuondoa hali ya sintofahamu kutokana na muda wa urais wa Dk Ali Mohamed Shein kuwa madarakani kuisha leo.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana makao makuu ya CUF, mjini hapa, Seif alisema yapo maendeleo mazuri ya kutatua mgogoro huo wa kisiasa visiwani kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa.
Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema, “kwa hiyo nawaomba wanachama na wafuasi wa CUF na Wazanzibari kwa ujumla, kuwa watulivu na wenye amani.” Kwa upande wake, Waziri Aboud alisema, 


Dk Shein ataendelea kuwa rais hadi hapo rais atakayechaguliwa, atakapoapishwa.
“Hii ni kupotosha watu kwa kusema kwamba Zanzibar haitakuwa na rais halali baada ya Novemba 2. Katiba ya Zanzibar kifungu cha 28 (1) A kiko wazi kwamba rais ataendelea kuwa madarakani hadi hapo atakapochaguliwa mwingine na kuapishwa,” alifafanua Aboud.
Alitaka viongozi wote wa vyama vya siasa, kuacha kutoa kauli ambazo zinaweza kusababisha vurugu huku akiwataka watangulize maslahi ya nchi. Wakati huo huo Kamishna wa Polisi, Hamdan Omar Makame alisisitiza juzi wananchi kuendelea na maisha yao ya kawaida.
“Hatutishi mtu yeyote, tunaomba watu waendelee na maisha yao ya kawaida,” alisema na kufafanua kwamba hali ya ulinzi waliyoiweka, ni kwa ajili ya kujiandaa kukabili uovu wowote unaoweza kutokea visiwani hapo. Aidha, Chama cha Wazee Zanzibar kimetaka wakazi wa visiwani humo kupuuza kauli za baadhi ya wanasiasa zinazochochea vurugu. “Zipo njia za kisheria na kidiplomasia za kutatua matatuzi, matumizi ya nguvu siyo njia nzuri,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Ali Hassan Khamis.
Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar”.


                                                Mwenyekiti wa ZEC Jecha Salim Jecha


Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa Sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”

No comments:

Post a Comment