Match Preview: Tanzania vs Algeria
                kikosi cha Timu ya Taifa Stars kikiwa mazoezini
TAIFA Stars kesho itakuwa ikisaka heshima kwenye uwanja wa nyumbani wakati itakapopambana na Algeria katika mchezo wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya kufuzufu fainali za Kom...
Algeria wanaoshika namba mbili kwa ubora Afrika wametinga moja kwa moja hatua ya pili baada ya kushiriki fainali za kombe la dunia lililopita ambalo lilifanyika Brazili na timu hiyo kutolewa hatua ya 16 bora.


Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa timu zote mbili kulingana na rekodi inavyoonyesha katika mechi zilizopita ingawa wageni Algeria wanapewa nafasi kubwa kwani kikosi chake kimesheheni wachezaji wenye uzoefu wa michuano mikubwa huku wakicheza kwenye timu za Ulaya.
Algeria tayari wamewasili nchini tangu jana jioni kwa ajili ya pambano hilo na leo wamefanya mazoezi yao ya mwisho kwenye uwanja wa taifa wakati Stars, iliyopiga kambi ya siku 10 nchini Afrika Kusini nayo imeshawasili nchini tangu juzi tayari kwa pambano hilo.
Kocha wa Stars mzawa Charles Boniface Mkwasa, amekiambia Goal, katika mchezo wa kesho anajivunia uimara wa kikosi chake hasa wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, ambao Jumapili ya wiki hii wameipa ubingwa wa Afrika klabu yao TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mkwasa amesema wanaingia kwenye mchezo huo wakijua fika wanakwenda kukutana na timu bora Afrika lakini hilo haliwapi hofu kutokana na maandalizi ambayo wameyafanya kwa muda wa wiki mbili ikiwemo kambi ya siku 10, nchini Afrika Kusini.
Algeria imekuja nchini ikiwa na kikosi cha wachezaji 24, wakiwemo 18, ambao wanacheza soka kwenye timu kubwa zinazoshiriki ligi mbalimbali Ulaya.
Kocha wa Algeria Christian Gourcuff, raia wa Ufaransa, ameonyesha hofu katika mchezo huo kwa kuamua kutumia nguvu nyingi kuongozana na jeshi la wachezaji wengi wa kimataifa kuja Tanzania.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa mwaka 2012, ikiwa ni katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika ambapo Tanzania iliweza kupata sare ya 1-1, katika pambano la kwanza lililopigwa Septemba 4, 2010 na Stars kuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Abdi Kassim kwa shuti kali la adhabu ndogo na baadaye wenyeji walisawazisha kwa shuti kali ambalo lilimshinda kipa Shaban Kado.
Katika mchezo wa marudiano uliopigwa uwanja wa taifa Dar es Salaam Algeria waliweza kushinda mabao 2-1 Mbwana Samatta akiwa mfungaji wa bao hilo moja la wenyeji.
Rekodi hiyo inaufanya mchezo huo kuwa mgumu licha ya Algeria kujiona inaweza kupata ushindi kirahisi kwani hata Tanzania nayo imeonyesha kubadilika sana baada ya miezi miwili iliyopita kuilazimisha sare ya 0-0, Nigeria na kisha kuitoa Malawi kwa jumla ya mabao 2-1, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya kufuzu fainali hizo.