Friday, 27 November 2015

Magazetin:Sherehe 30 mikononi mwa Magufuli




Dar es Salaam. Sherehe 30 za maadhimisho ya kitaifa zinazofanyika nchini kila mwaka huenda ‘zikachinjwa’ kutokana na kasi ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli ya kupunguza gharama na kubana matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.
Wasiwasi wa kufutwa kwa maadhimisho hayo ya kitaifa umekuja baada ya Rais Magufuli juzi kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyopangwa kuadhimishwa Desemba Mosi kabla ya hapo, alifuta sherehe za Uhuru ambazo zingefanyika Desemba 9.
Rais aliagiza kuwa fedha zitakazotumika kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, zitumike kununua dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV) na zile za Siku ya Uhuru zitumike kwa usafi wa mazingira ili kupambana na kipindupindu.
Katika mwendelezo huo, jana Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipiga marufuku utengenezaji na uchapishaji wa kadi za Krismasi na Mwaka Mpya kwa gharama za Serikali.
Katika taarifa yake, Balozi Sefue ameelekeza kuwa yeyote anayetaka kutengeneza au kuchapisha kadi hizo, afanye hivyo kwa gharama zake na ameagiza fedha zilizopangwa kugharamia utengenezaji na uchapishaji huo, zitumike kupunguza madeni ambayo wizara, idara na taasisi za umma zinadaiwa na wananchi na wazabuni waliotoa huduma kwao au zipelekwe katika matumizi mengine ya kipaumbele.
Sherehe sasa kwa vipaumbele
Akizungumzia kufutwa kwa maadhimisho ya sherehe za kitaifa, Sefue alisema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo kwa mamlaka aliyonayo kisheria na kuwa hatua hiyo si endelevu, bali kwa kuangalia vipaumbele.
Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35), inampa Rais mamlaka ya kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko.
Kutokana na sheria hiyo, ndiyo maana Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alitangaza Novemba 5 mwaka huu, kuwa ya mapumziko katika kuhitimisha uongozi wa awamu ya nne na kuukaribisha wa awamu ya tano.
“Maadhimisho haya yana umuhimu lakini si lazima yafanyike kila mwaka, tunaweza kuamua mwaka huu tufanye au turuke mwaka mmoja. Siku ya Ukimwi ina umuhimu na siku ya Uhuru ina umuhimu pia, lakini tunapima kwa kuangalia wapi kuna mahitaji zaidi,” alisema.
Alisema uamuzi huo wa Rais ni njia mpya ya kupanga vipaumbele kutokana na hali halisi ilivyo katika sekta zenye mahitaji makubwa na ya haraka.
Katika hotuba yake ya kuzindua Bunge ya Novemba 20, Rais Magufuli alisema Serikali itadhibiti warsha, semina, makongamano na matamasha ambayo yanatumia fedha nyingi za lakini hayana tija.
Alisema atahakikisha kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
“Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi,” alisema katika hotuba hiyo.
Baadhi ya maeneo ambayo alisema yatasimamiwa ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali ni kufuta safari za nje, posho za kujikimu na kodi.
Wazungumzia kasi ya Magufuli
Hatua hiyo ya Rais Magufuli, imepongezwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati.
Aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Segerea, Julius Mtatiro alisema Rais alitakiwa kuandaa utaratibu wa kufuta sherehe hizi kila mwaka ili fedha zitumike katika sekta nyingine za kimaendeleo.
“Niliposikia amefuta nilidhani ni kwa miaka yote kumbe ni mwaka huu tu, inawezekana labda ni kwa sababu Serikali haina fedha na wala si kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,” alisema.
Alisema sherehe hizo ni vyema zikafutwa kabisa kwani hazileti maana kutumia fedha nyingi wakati wanawake wanajifungulia sakafuni na watoto wanaketi chini madarasani.
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Hakielimu, Godfrey Bonaventure alipongeza hatua ya Rais Magufuli huku akitaka hatua hiyo iwe endelevu.
“Afanye hivi miaka yote, tumekuwa na utaratibu usiopendeza ambao Serikali inakuwa na matumizi yasiyo ya lazima,” alisema.
Alisema anachofanya Rais Magufuli ni kutumia kile kidogo kilichopo na kukiwekeza katika maendeleo badala ya kutumika katika matumizi yasiyo na tija.
Bonaventure alimtaka pia kufuta sherehe za kupongezana baada ya bajeti kupita na mambo mengine yasiyo na msingi.
“Masuala ya safari, semina, vikao na ‘overtime’ fedha huwa zipo lakini masuala muhimu siku zote tunaambiwa fedha hazitoshi, kwa nini?” alihoji Bonaventure.     

No comments:

Post a Comment