Tuesday 8 December 2015

MAGAZETINI--Wafanyakazi kula kiapo cha uadilifu


Dar es Salaam.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imemtaka kila mtumishi wa umma nchini kuapa kiapo cha ahadi ya uadilifu kabla ya Desemba 31, kwa kukisoma mbele ya mwajiri wake huku akishuhudiwa na wenzake.
Utaratibu wa utekelezaji wa ahadi ya uadilifu kwa watumishi wa umma ulitolewa kupitia waraka wa mkuu wa utumishi wa umma, namba 2 wa mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa ahadi ya uadilifu kwa viongozi, watumishi wa umma na sekta binafsi wa Agosti 1, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hab Mkwizu, alisema kila mwajiri atapanga muda unaofaa kwa watumishi walio chini yake kutoa ahadi ya uadilifu kwa kusoma kwa sauti yaliyomo kwenye fomu huku wakishuhudiwa na wenzao.
Wakurugenzi watendaji na maofisa wa uchaguzi
“Zoezi hili litafanyika mara moja kwa kila mtumishi na kila kiongozi wa umma na kurudiwa pale mtumishi au kiongozi wa umma anapopandishwa cheo au kuhamishwa kwa mwajiri mwingine. Watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza watatakiwa pia kutoa ahadi ya uadilifu,” alisema.
Mkwizu aliongeza kuwa waajiri wote walioelekezwa kutekeleza jambo hili katika utumishi wa umma ni makatibu wakuu, wakuu wa idara zinazojitegemea, wakala wa serikali, makatibu tawala wa mikoa na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa.
Aliwataja waajiri wengine waliopewa maelekezo hayo kuwa ni katibu wa Bunge, mtendaji mkuu wa mahakama na mashirika ya umma.
“Ahadi ya uadilifu itakuwa ni sehemu ya masharti ya ajira na upandishwaji vyeo katika utumishi wa umma na mashirika ya umma,” alisema Mkwizu na kusisitiza kuwa hili siyo jambo jipya kwa sababu mchakato wake ulianza zamani.
Alisema makatazo yaliyomo katika kiapo (ahadi ya uadilifu) hicho ni pamoja na watumishi wa umma kutakiwa kujiepusha na ubaguzi wowote, kuomba au kutoa rushwa, kutumia madaraka kwa manufaa binafsi, kutoa siri za Serikali na kuepuka tabia inayovunja heshima ya utumishi wa umma.

No comments:

Post a Comment