Thursday, 24 December 2015

Serikali imezipongeza taasisi za elimu ya juu za umma na za binafsi kwa kutoa fursa zaidi za masomo kwa vijana



Serikali imezipongeza taasisi za elimu ya juu za umma na za binafsi kwa kutoa fursa zaidi za masomo kwa vijana wa Zanzibar na kutoka nje na kwamba hiyo ni hatua nzuri na muhimu kwa mustakabala wa Zanzibar.

Akizungumza katika mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar huko Tunguu nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika kuendeleza elimu nchini umeleta mafanikio makubwa.

“Serikali imefurahishwa kuona taasisi binafsi za elimu kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu zimeongezeka kwa kasi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita” alisema Dk. Shein na kuongeza kuwa taasisi hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa serikali.

Aliieleza jumuiya ya wanachuo na wageni waliohudhuria mahafali hayo kuwa ameridhishwa kuona kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la vijana wa Zanzibar wanaojiunga na elimu ya juu ndani na nje ya nchi na kueleza kuwa huo ni mwelekeo mzuri kwa taifa.

“Naupongeza sana mwamko huu wa vijana kuchangamkia elimu ya juu kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa elimu ni msingi wa taifa bora na lenye ustawi hivyo naamini kwa dhati kuwa mustakabala wa Zanzibar unategemea hizi jitihada zetu katika kuwaelimisha vijana” Dk. Shein alisisitiza.

Katika mnasaba huo ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar kwa kuongeza udhamini wa nafasi za masomo kwa vijana wa Zanzibar kutoka 55 hadi 100 kwa mwaka na kueleza kuwa huo ni mfano unaopaswa kuigwa na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini.

Dk. Shein alibainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa taasisi za elimu ya juu nchini katika maendeleo ya Zanzibar na watu wake kwa taasisi hizo kuendelea kutoa wahitimu bora ambao wameweza kupata mafanikio katika sehemu mbalimbali wanazotekeleza wajibu wao.

Katika hotuba yeka hiyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa pamoja na kuwepo mafanikio katika kujenga mazingira bora na ya usawa kati ya watoto wa kike na wa kiume katika elimu, Serikali itaendelea kuchukua hatua zas kuimarisha mazingira hayo ili kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike.
“Serikali imeweka mikakati ya kuimarisha hali ya wanawake kielimu, afya na kuwa uwezo kwa madhumuni ya kulinda haki na kutoa fursa kwa wanawake kote nchini katika harakati za maendeleo ya kiuchumi na kijamii” Dk. Shein alisisitiza.
Alibanisha kuwa baadhi ya matunda ya hatua hizo ni namna ambavyo vijana wa kike wanavyopata fursa za kujiunga kwa wingi na elimu kuanzia ngazi ya chini hadi elimu ya juu na wamekuwa wakionesha uwezo mkubwa ambapo mara kwa mara wamekuwa wakishika nafasi za juu kuliko vijana wa kiume.

Kwa upande wa wahitimu amewataka kuitumia vyema elimu waliyopata kwa kutumia fursa zilizopo za kujipatia kipato na zaidi wajiandae kukabiliana na changamoto za maisha.

“Muzichukue changamoto kama fursa kwenu kwani zitawasaidia kuwajenga na kuongeza uwezo kwa kuwa maisha ni safari iliyojaa changamoto ambazo kila mwanadamu anapaswa kujiandaa kukabiliana nazo” Dk. Shein aliwasihi wahitimu hao.

Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu wahitimu 678 wa ngazi ya vyeti (254), Diploma (33), 349 shahada za kwanza na 42 shahada za uzamili katika fani mbalimbali walitunukiwa vyeti vyao na Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Mwenyekti wa Bodi y Wadhamini ya Chuo Profesa Suleiman Bin-Nasry Basahal.

Akizungumza katika mahafali hayo Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Mustafa Roshash, alieleza kuwa uongozi wa chuo unaendelea na jitihada zake za kuimarisha taaluma chuoni hapo kwa kuendelea kusomesha wakufunzi wake katika kiwango cha shahada za uzamivu.

Alibainisha kuwa chuo hicho kinatoa kozi 8 ngazi ya cheti, 8 ngazi ya diploma, 14 ngazi ya shahada ya kwanza, shahada za uzamili 4 na moja ya Uzamivu.
Profesa Roshash alieleza pia kuwa wanafunzi chuoni hapo wanatoka Zanzibar,Tanzania Bara na nchi za Malawi, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Botswana, Ethiopia, Sudan, Nigeria na Afrika Kusini.

Alifafanua kuwa tangu kuanzishwa kwake chuo hicho mwaka 1998, kimetoa wahitimu 5791 kati yao wahitimu 3042 ni wanaume ambao ni asilimia 52 wakati wahitimu waliobaki 2749 ambao ni asilimia 48 ni wanawake

No comments:

Post a Comment