Monday 18 April 2016

Athari za Mvua visiwani Z’bar familia kadhaa zakosa makazi baada ya nyumba 25 kuanguka

Screen Shot 2016-04-18 at 2.50.16 PM
Nyumba zipatazo 25 katika jimbo la Chumbuni, Mkoa wa Mjini Maghrib zimeanguka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha familia kadhaa kukosa makazi na nyingine kulazimika kupata hifadhi kwa jamaa na majirani katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar.


Mvua hizo ambazo zinanyesha kwa siku ya nne mfululizo, mbali na kuathiri makazi ya watu pia zimeathiri miundombinu ya barabara na kulazimika baadhi ya njia kufungwa na nyingine kupitika kwa shida kutokana na kujaa maji ya mvua.

Wakizungumza na Channel Ten baadhi ya waathirika wa mvua hizo katika jimbo la Chumbuni,liliopo katika Mkoa wa Mjini Maghrib wamesema wanaishi katika mazingira magumu na msaada wa serikali unahitajika haraka ili kuwapunguzia ukali wa maisha na usumbufu wanaoupata hivi sasa baada ya nyumba zao kuvamiwa na maji.

Tatizo la nyumba kuvamiwa na mafuriko ya maji limekuwa la kawaida kila wakati wa msimu wa mvua zinaponyesha kutokana na ramani ya mipango miji katika mji wa Zanzibar kuathiriwa na ujenzi holela unaochangiwa na urasimu wa upatikanaji wa viwanja vya kupima na wanyonge kulazimika kujenga mabondeni na katika vianzio vya maji.

No comments:

Post a Comment