Sunday 17 April 2016

Kamati ndogo ya Uchunguzi yabaini kutafunwa Shs.bil 5 katika stendi kuu ya mabasi ubongo Dar es salaam

 ubungo
Uchunguzi uliofanywa na Kamati ndogo kuhusu Makusanyo ya Mapato na mikataba ya Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam katika Stendi kuu ya mabasi Ubungo jijini huo umebaini kuwa kiasi cha Shilingi Billioni 5 zimetafunwa na baadhi ya watu kupitia Mikataba na ukusanyaji kodi katika Stendi hiyo.

Aidha kamati hiyo imeanisha ubadhirifu mwingine ambao unaashiria kuwepo kwa Vitendo vya rushwa kwa kuongeza mikataba kinyemela ni pamoja na kumpa mzabuni kazi ya ukusanyaji mapato bila kutangazwa wazi kwa zabuni husika, huku pia kampuni ya uegeshaji magari ya National Parking System pamoja na Kampuni ya Tambaza nazo zikidaiwa kuhusika katika mikataba iliyokiukwa kisheria.

Mkuu wa Mkoa wa DSM akizungumza na waandishi wa habari ametangaza hadharani kutokuwa tayari kuendelea na kazi na Mkurugenzi wa jiji Wilson Kabwe pamoja na timu yake huku akisema suala hilo tayari liko mikononi mwa viongozi wa juu wa nchi pamoja na Takukuru kwa Uchunguzi.

Aidha Kamati ya Uchunguzi imebaini ukodishaji wa Vyumba vya ofisi ambapo kwa mujibu wa mkataba wa jiji mpangishwaji anapaswa kulipa laki moja kwa mwezi lakini wajanja wachache hukodisha shilingi millioni moja laki mbili mpaka laki sita kwa mwezi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa kamati hiyo, Kampuni ya udalali ya Tambaza iliyopewa zabuni ya kukamata magari na pikipiki ilitakiwa kutoza faini isiyopungua shilingi elfu ishirini lakini imekuwa ikitoza shilingi elfu 80 hadi lakini mbili fedha ambazo hazijulikani zinakwenda wapi.

No comments:

Post a Comment