Sunday 17 April 2016

Kauli Raisi Magufuli kuhusu misaada yenye masharti

 
RAIS John Magufuli amefungua mdomo kuhusu misaada ya nchi wahisani inayoambatana na masharti, aliyoipa jina ‘mkate wa masimango’ na kusema kuliko kula mkate huo ni bora kushindia muhogo.

 Alisema hivyo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (Flyover), inayojengwa katika makutano ya Barabara za Mandela na Nyerere, kwenye eneo la Tazara. Barabara hizo zinajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuzungumzia misaada yenye masharti tangu Shirika la Changamoto ya Milenia (MCC) la Marekani, kusitisha msaada wa Dola za Marekani milioni 472.8 sawa na karibu Sh trilioni moja, zilizokuwa zitumike kuongeza kasi ya usambazaji umeme.

MCC ilisitisha msaada huo pamoja na uhusiano wake na Serikali ya Tanzania kwa madai kuwa Serikali haijachukua hatua za kuheshimu uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao.

Bodi ya shirika hilo ilisema Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio Zanzibar, ambao haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya wote, licha ya malalamiko kutoka kwa Serikali ya Marekani na jamii ya kimataifa.

Akionesha kukerwa na misaada inayoambatana na masharti, Rais Magufuli aliisifu Japan kuwa ni rafiki wa kweli wa Tanzania, kwani imekuwa ikitoa misaada isiyo na masharti na kuongeza kuwa, nchi rafiki za aina hiyo ziko nyingi na zimejitokeza kutoa misaada isiyo na masharti.

Katika ujenzi wa barabara hizo, kwa mujibu wa Rais Magufuli, Japan imeshatoa fedha za walipakodi wake Sh bilioni 93.44 na Tanzania imeshatoa Sh bilioni 8.3 na kufanya mradi huo kugharimu zaidi ya Sh bilioni 100.

Rais Magufuli alisema, kwa kuwa fedha zipo na mkandarasi na mhandisi mshauri ni wazoefu wa ujenzi wa barabara za aina hiyo duniani, huenda zikakamilika kabla ya Oktoba 2018.

“Nawashukuru sana, (Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida), fikisha shukrani nyingi kwa Serikali ya Japan kwa jinsi wanavyotusaidia katika miradi mbalimbali kwani tunaposaidiwa na nchi tajiri, maana yake ni kuwa wamechukua fedha za walipakodi wao na kuamua kuleta Tanzania ambapo hatutaki kulipa kodi,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, kwa kuwa Japan imetumia fedha za walipa kodi wake kuisaidia Tanzania, Rais Magufuli alitoa mwito kwa Watanzania kuhamasishana kulipa kodi ili katika miradi mingi ya maendeleo, nchi ijihimili yenyewe. Alihakikishia nchi wahisani kwamba hakuna fedha ya misaada itakayopotea na kusisitiza kuwa Serikali yake imeamua kujisimamia yenyewe.

No comments:

Post a Comment