Tuesday 26 April 2016

Kauli ya Ole Sendeka kwa Rais Magufuli kuhusu wakwepa kodi

 
Msemaji wa chama cha mapinduzi Christopher Ole Sendeka amemuomba Rais Magufuli kuwaanika hadharani wanaokwepa kulipa kodi nchini

Sendeka alisema hayo jana wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa madiwani na viongozi wakuu wa CCM katika kata zote za Manispaa ya Morogoro.

Aidha, alimshauri Rais Magufuli, kama anavyofanya kuwabaini watumishi hewa na kuwashugulikia, apige hatua mbele zaidi katika eneo hilo la bandari kwa kuwaanika ili kuijengea heshima CCM na kurejesha imani kwa wananchi ambao wana matumaini makubwa kwake.

Aliwaomba wanaCCM wote na Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono kuwabaini watu wote ambao wanasababisha kuwapo kwa ubadhilifu unaopelekea nchi kushindwa kuendelea.

‘’Mimi nimeamua kumuunga mkono Rais hata akimtumbua ndugu yangu wa tumbo moja, na nyie nawaomba hata kama ndugu yako anatumbuliwa inabidi uvumilie na umuunge mkono ili aweze kufanya kazi yake vizuri na kuleta manufaa kwa wananchi walio wengi,’’ alisema.

Alisema hakuna yeyote anayeogopwa katika Serikali ya Magufuli, alimwomba kuendelea kusafisha safu ya watendaji wa serikali kwa kuwaondoa wote walioonyesha kuwapo kwa harufu ya ufisadi.
Alisisitiza kuwa kama kuna mwana CCM alifanya ubadhirifu huo, na anayo kadi ya CCM anatakiwa kuhukumiwa mara mbili, 
kuvunja sheria ya nchi na kukiuka ahadi za mwanachama wa CCM.
“Lazima tuifanye CCM iwe kimbilio la wanyonge, chama kirudi katika uasili wake, kazi anayofanya Magufuli sio tu ya kufanya CCM iendelee kushinda mwaka 2020, bali pia anaweka msingi wa kuasisiwa,’’ alisema.

Aidha, aliwataka viongozi wa CCM kuacha kutumia mianya ya makundi ya urais kuwahukumu watu waliokuwa katika kambi mbalimbali na badala yake waangalie baada ya uchaguzi yupo aliyesaliti ndio wanastahili kuchukuliwa hatua.

“Wakati wa mchakato wa U-rais kila mmoja alikuwa katika kambi yake, na baada ya uchaguzi wote wanatakiwa kuwa pamoja, sasa wapo viongozi ambao wanatumia kigezo hicho kuwahukumu watu ambao wanajua ni tishio kwao wanapotaka kugombea hiyo sio sahihi,’’ alisema.

Kwa upande wake Katibu wa CCM, Wilaya ya Morogoro, Kulwa Milonge, alisema katika kuhakikisha chama kinafuata nyayo za Rais Magufuli, wameweka utaratibu wa kusikiliza kero za wanachama na wananchi siku moja kwa wiki na kuzifanyia kazi.

Pia akisema ili kumuunga mkono Rais katika harakati zake za kuboresha elimu, CCM wilaya imeandaa mkakati wa kutafuta madawati 4000 kwa ajili ya kusaidia shule za Manispaa ya Morogoro.

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo viongozi hao ili kufanya kazi zao kwa ufasaha.

No comments:

Post a Comment