Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe alikutana na Askofu mkuu wa Canterbury na kuibua maswali kuhusu ndoa za wapenzi wa jinsia moja.
Askofu mkuu Justin Welby amesema alimjibu kiongozi huyo kwamba kuna mitazamo tofauti kuhusu ndoa hizo miongoni mwa waumini wa kanisa la Kianglikana kote duniani.
Aliongeza hata hivyo kwamba wengi wa waumini wanaamini ndoa ni uhusiano wa muda mrefu baina ya mwanamume na mwanamke.
Askofu Welby alisema ni makosa kuwahukumu au kuwaadhibu watu kwa sababu ya msimamo wao kijinsia na kimapenzi.
Hata hivyo, amesema dalili zilionesha Bw Mugabe hakukubaliana naye.
“Sidhani itakuwa haki kusema kwamba Bw Mugabe alikubaliana nami kabisa,” alisema Askofu Welby.
Mkutano huo wa faraghani ulifanyika mjini Harare, baada ya Askofu Welby, ambaye yumo katika taifa jirani la Zambia anakohudhuria mkutano wa viongozi wa kanisa la Kiangilikana kufanya ziara fupi Zimbabwe.
Msemaji wa Lambeth Palace amesema mpango huo ulipangwa dakika za mwishomwisho na ulidumu chini ya saa moja.
Bw Mugabe ni Mkatoliki na hupinga sana ndoa za wapenzi wa jinsia moja.
Mwandishi wa BBC Callum May anasema mkutano huo ndio wa kwanza kufanyika kati ya askofu mkuu wa kanisa la Kiangilikana na Bw Mugabe tangu 2011 uhusiano kati ya kanisa hilo na serikali ulipokuwa umedorora sana.
Askofu Welby amesema hali kwa sasa imeimarika sana.
Suala la kutambuliwa kwa ndoa wapenzi wa jinsia moja limekuwa likizua mgawanyiko hasa katika kanisa la Kianglikana duniani, zikipingwa sana na majimbo ya kanisa hilo barani Afrika..
Januari mwaka huu viongozi wa kanisa hilo waliokutana Canterbury, walisisitiza kwamba ndoa ni kati ya mwanamume na mwanamke na likasimamisha ushirika wa jimbo la Marekani lililotambua ndoa za wapenzi wa jinsia moja.
Walisema kanisa hilo lilikiuka Imani inayofuata na waumini wengi wa kanisa la Kianglikana kuhusu ndoa.
No comments:
Post a Comment