Tuesday 19 April 2016

Uzinduzi wa Daraja la Kigamboni kufanyika leo na Raisi Magufuli(+picha)


             Muonekanao wa Daraja nyakati za usiku
Rais John Magufuli leo anatarajiwa kulifungua daraja la kulipia la Kigamboni na kuweka historia mpya ya miundombinu ya kisasa ya barabara nchini.

Daraja hilo lililochukua miaka minne mpaka kukamilika kwake, limegharimu Sh214.6 bilioni zilizotokana na vyanzo vya ndani kwa ushirikiano wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Wakala za Barabara (Tanroads) chini ya Wizara ya Ujenzi.

Mhandisi mshauri kutoka NSSF anayesimamia mradi huo, Kareem Mattaka alisema kuwa licha ya kufunguliwa leo, wananchi wataendelea kutumia bure mpaka hapo baadaye mamlaka husika zitakapokubaliana juu ya kiasi kinachostahili.

Mradi huo unaojengwa kwa ushirikiano wa kampuni mbili za ukandarasi, China Railway Major Bridges Engineering Construction Limited (MBECL) na China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) ulianza kutekelezwa mwaka 2012.
 
Awali ulitarajiwa ukamilike Januari mwaka jana, lakini kutokana na sababu kadhaa zilizojitokeza umekamilika mwezi huu na matumizi yake yanaanza rasmi leo, hivyo kuiingiza Tanzania kwenye orodha ya mataifa kadhaa yenye madaraja ya kulipia.

Daraja lenyewe lina urefu wa mita 680. Kati ya hizo mita 400 zinashikiliwa na nyaya zinazohimili uzito wa daraja na uzito wowote utakaokuwa juu yake pindi linapoanza kutumika. Urefu uliobaki umejengwa kwa teknolojia ya maboksi.

Kitako cha daraja kinashikiliwa na nguzo ambazo zimezamishwa baharini. Urefu wa nguzo hizo ambazo kipenyo chake ni kati ya mita moja mpaka moja na nusu ni kilomita 11.5. Daraja limeunganishwa na barabara yenye urefu wa kilomita 2.5, moja upande wa Kurasini na kilomita 1.5 Kigamboni.
 

Barabara ya Kurasini inayoruhusu magari kupita chini ya reli inayotoka bandarini na mbele kidogo kuna barabara ya juu ambayo haitoi mwanya wa magari yanayotumia ile ya Mandela kukutana na yanayotoka Kigamboni na kusababisha foleni.
Daraja hili lililosimamiwa na kushauriwa kitaalamu na kampuni ya M/s Arab Consulting Engineers kutoka Misri lina upana wa mita 32.5.
Daraja lina njia sita za magari na moja ya waenda kwa miguu kila upande. Kati ya mita 32.5 za daraja hilo tano ni za waenda kwa miguu ikiwa ni mita 2.5 kushoto na 2.5 kulia.




Kigamboni vipo vibanda 14 vya malipo. Ikumbukwe kuwa daraja ni la kulipia. Saba kila upande wa njia tatu za magari. Yapo pia majengo kwa ajili ya shughuli za utawala.

Kabla ya vibanda vya kulipia kuna majengo saba ambayo yana ofisi za utawala, huduma ya kwanza, kituo cha polisi na Jeshi la Zimamoto, ofisi ya wahandisi na maabara, chumba cha jenereta, mizani za pande zote mbili na kituo cha malipo.

Mattaka alisema kukamilika kwa majengo yote kutaruhusu biashara kwa ajili ya wananchi watakaokuwa wanavuka daraja hilo: “Daraja litakuwa na ulinzi wa kutosha ili kukabiliana na wizi au biashara zisizo rasmi. Wale watakaokidhi vigezo watapewa nafasi kwenye majengo yatakayojengwa kwa ajili hiyo.”

Mradi huo ulianza kutumika Aprili 16 bila malipo yoyote baada ya Wizara ya Ujenzi kuruhusu suala hilo baada ya ujenzi kukamilika kwa kiasi kikubwa. 

No comments:

Post a Comment