Monday 18 April 2016

Viongozi wa CUF waliopo Kizuizini Zanzibar Mahakama kuu yataka maelezo ya Polisi

 
Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mkusa Isack Sepetu ametoa muda wa saa 24 kwa Jeshi la polisi Zanzibar kuwasilisha sababu zinazowafanya kuendelea kuwashilikia watuhumiwa wanne wakiwemo viongozi watatu wa Chama cha Wananchi (CUF), bila ya kuwafikisha Mahakamani tangu walipokamatwa April 16
mwaka huu kwa tuhuma za kuripua nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame.
Jaji Mkusa ametoa agizo hilo, kufuatia ombi lililofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar  na Wakili anayewatetea watuhumiwa hao, Rajab Abdallah Rajab kufuatia wateja wake kuendelea kuwepo kizuizini katika kituo cha Polisi cha Mwembe Madema tangu walipokamatwa April 16, mwaka huu.
Screen Shot 2016-04-18 at 6.08.54 PMWatuhumiwa waliokamatwa ni Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Maghrib A, Hassan Omar Issa, Katibu wa CUF Wilaya ya Maghrib A, Saleh Mohamed Saleh ambaye pia ni Mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Katibu wa CUF jimbo la Mfenesini Suleiman Mohamed Bakari pamoja na Omar Bakari Nassor ambao wanaendelea kushikiliwa na Jeshi hilo la polisi kwa muda wa siku 20 tangu walipokamatwa.
Wakili huyo ameiomba Mahakama hiyo kutambua kuwa wateja wake wananyimwa uhuru wa kikatiba kwa kuwa huru na kufanya shughuli nyingine, wakati bado hawajatiwa hatiani na mahakama na kitendo cha kukaa nao bila ya kuwafikisha katika vyombo vya sheria ni uvunjaji wa sheria na haki za binadamu.
Hata hivyo Mkuu wa kitengo cha sheria na utafiti kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar Ramadhan Hassan Jabu amesema ombi hilo lililofunguliwa mahakamani hawakupatiwa hoja wanazotakiwa kuzijibu kwa wakati na kuomba Mahakama iwape muda ili waweze kujipanga kuieleza mahakama kwa nini wanaendelea kuwashikilia watuhumiwa hao bila ya kuwafikisha mahakamani.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mkusa Isac Sepetu amesema kwa kuwa Polisi wamepokea barua ya wito wa kufika mahakamani ikieleza na madhumuni ya wito, walipaswa kufahamu wanachoitiwa na kujiandaa kwa maelezo, na hivyo kuwapa muda wa siku moja kufika Mahakamani April 19, saa tatu asubuhi na kuieleza Mahakama kwa nini wanaendelea kuwaweka kizuizini watuhumiwa hao bila ya kuwafikisha Mahakamani au kuwapatia dhamana.
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za kula njama kuripua kwa bomu nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame, pamoja na kupanga mipango ya kuripua kwa bomu nyumba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na nyumba ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai.

No comments:

Post a Comment