Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo imeshindwa kutoa uamuzi kuhusu dhamana kwa watuhumiwa Harry Kitilya na wenzake wawili Shose Sinare na Sioi Solomon kutokana na jalada la kesi yao kuitishwa mahakama kuu kanda ya Dar es salaam.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Emilious Mchauru amesema uamuzi huo hauwezi kusomwa kutokana na jalada halisi la kesi hiyo kuwasilishwa mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam asubuhi ya leo na hivyo kuamuru watuhumiwa warudishwe mahabusu mpaka kesi yao itakapotajwa tena Mei 03 mwaka huu kufuatia agizo la Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwamba kesi hiyo itajwe Mei 3 badala ya badala ya Mei 12 mwaka huu iliyokuwa imepangwa awali wakati watuhumiwa hao walipopandishwa kizimbani leo.
Aprili 27 mwaka huu Hakimu Mkazi Mfawidhi Emilious Mchauru alifuta shtaka la nane la utakatishaji fedha lililo katika kesi inayowakabili kamishna mkuu wa Zamani wa Mamlaka ya Mapato Harry Kitilya na wenzake Shose Sinare na Sioi Solomoni.
Hata hivyo kufuatia uamuzi huo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), aliwasilisha hati ya mapendekezo ya kukata rufaa kupinga uamuzi wa kulifuta shtaka hilo ambalo limekuwa likiwanyima fursa watuhumiwa ya kupata dhamana.
April 1 mwaka huu Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa Tanzania TAKUKURU iliwapandisha kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu Harry Kitilya na wenzake kwa makosa ya kula njama ya kujipatia fedha kwa udanganyifu kwa lengo la kuiwezesha serikali ya Tanzania kupata mkopo wa dola za kimarekani milioni 550 kutoka ya Standard Bank ya London kupitia na Benki ya Stanbic Tanzania.
No comments:
Post a Comment