Friday, 22 April 2016

Magazetini:Kasi ya Magufuli yatinga bungeni

 
FALSAFA ya Rais John Magufuli ya Hapa Kazi Tu imeanza kutekelezwa bungeni baada ya jana, Bunge kutengua baadhi ya kanuni zake ili wawe na muda mwingi zaidi wa kufanya kazi; kitendo ambacho Spika wa Bunge ameomba Watanzania wote kufuata nyayo za mhimili huo.

Aidha, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano umepitishwa na Bunge, huku wabunge wakieleza kuwa na imani kubwa ya kutekelezwa kwa kile kilichoelezwa ni nidhamu iliyojengwa kwa muda mfupi na Rais Magufuli katika utumishi wa umma.
Uamuzi wa kuongeza muda wa majadiliano kutoka saa 10 hadi saa 2 usiku, ulipitishwa jana na wabunge baada ya hoja husika kuwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama.
Waziri Mhagama aliwasilisha pia pendekezo la serikali la kutengua kanuni Bunge liendelee na vikao vyake Jumamosi badala ya kusitisha Ijumaa.
Pia alipendekeza Mawaziri kupewa dakika 45 kusoma hotuba zao za bajeti na dakika 50 wakati wa kuhitimisha hotuba hizo. Kanuni za Bunge zinalitaka Bunge kuanza vikao vyake saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana ambapo husitishwa na kurejea saa 11:00 jioni mpaka saa 2:15 usiku.
Pia kanuni za Bunge zinalitaka Bunge kusitishwa Ijumaa hadi Jumatatu.
Akijenga hoja hiyo iliyopitishwa kwa kishindo na Bunge, Waziri Mhagama alisema lengo ni kuwezesha Bunge kufanya kazi kubwa zaidi na kukamilisha kazi zote za Bajeti itakayosomwa Juni 9 mwaka huu katika muda muafaka sawa na mabunge mengine ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Kwa kuzingatia kwamba vikao vya Mkutano huu wa Bunge vilianza Aprili 19 mwaka huu na kwa vile vitaendelea hadi Julai Mosi, mwaka huu, Bunge linalazimika kutengua baadhi ya kanuni zake ikiwepo kanuni ya 105, ili kuweza kumaliza kazi zake katika muda uliopangwa,” alisema Waziri Mhagama.
Akizungumza mara baada ya Bunge kutengua kanuni hizo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema mabadiliko hayo yanalenga kuliwezesha Bunge kuendana na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu’.
“Nawashukuru sana wabunge kwa kukubali kwa kauli moja kutenguliwa kwa kanuni hizi za Bunge ili kutupa muda mwingi zaidi wa kuchapa kazi na nawaomba Watanzania wote waige mfano huu wa Bunge wa kumuunga mkono Rais katika suala la uchapaji kazi,” alisema Ndugai.
Imani kwa JPM
Kabla ya kupitishwa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wabunge wengi walisema wana imani kubwa ya utekelezaji wa mpango huo.
Mambo yaliyowaaminisha wabunge wengi yaliegemea katika nidhamu ya matumizi ya umma, ulipaji wa kodi, mawaziri kuiga utendaji wa Rais, ufuatiliaji katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo maji, kilimo, afya, elimu, miundombinu na uwajibikaji uliohuishwa serikalini.
Wakati Mpango wa miaka mitano unaomalizika wenye thamani ya Sh trilioni 44.5 umetajwa kutekelezwa na serikali kwa kiwango cha asilimia 60 , wabunge wengi wamesema wana imani na Mpango huo wa awamu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli wenye thamani ya Sh trilioni 107, utatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Wakijadili mpango huo uliowasilishwa juzi na kuhitimishwa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, wabunge walisema kwa namna Dk Mipango alivyoainisha vipaumbele vya maendeleo ni wazi kwamba sasa dira ya kulifikisha taifa katika uchumi wa kati inaonekana dhahiri.
Mbunge wa Kisesa, Dk Raphael Chegeni (CCM) alisema nidhamu ya uwajibikaji serikali, ikiwa ni pamoja na kasi ya utumbuaji wa majipu ambayo imewafanya Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kuwajibika na kuogopa kujihusisha na rushwa na ufisadi hatua itakayolipaisha Taifa.
“Mheshimiwa Spika, sekta ya umma ni tatizo kubwa katika nchi hii na dawa pekee ni utumbuaji wa majipu, ni lazima Watanzania wote tumuunge mkono kwa nguvu zetu zote Rais Magufuli katika utumbuaji wa majipu, kila mahali yalipoota ni lazima yatumbuliwe nchi iende,” alisema Dk Chegeni.
Akizungumzia nidhamu katika ulipaji wa kodi, Mbunge huyo alisema ndani ya muda mfupi nidhamu katika kulipa kodi imeanza kurejea tofauti na zamani ambapo wafanyakazi ndio waliokuwa wakilipa kodi huku wafanyabiashara wakiona suala la kulipa kodi ni sawa na uzembe.
Alisema mfano wa wazi kabisa unaodhihirisha utekelezaji wa Mpango huo ni hatua ya kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kutoka Sh bilioni 850 hadi Sh trilioni 1.3 kwa mwezi katika uongozi wa Rais Magufuli, lakini akasema ni lazima mianya zaidi katika ukwepaji wa kodi idhibitiwe huku akizitaja kampuni za simu kuhusika kwa kiasi kikubwa na ukwepaji wa ulipaji wa kodi halali za serikali.
“Mheshimiwa Spika hili la kampuni za simu ni lazima tulitafutie dawa. Nakumbuka TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania), iliwahi kuwaeleza TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) namna ya kukusanya kodi kwa kampuni za simu. Ni lazima mfumo uliopo ubadilishwe haraka ili kuzuia ukwepaji kodi. “Ukiondoa ukwepaji kodi katika biashara zao lakini pia kuna hili suala la minara ya simu. Minara hii imejengwa kila mahali vijijini, lakini halmashauri za wilaya hazinufaiki na uwepo wa minara hii, wakati umefika sasa wa kulitazama upya hili,” alisema Chegeni.
Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM), Mbunge wa Mbogwe Agustino Masele (CCM), Mbunge wa Busanda, Lolensia Bukwimba (CCM), Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema) walijielekeza zaidi katika kuishauri serikali kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo maji, elimu, afya, miundombinu na kilimo.
Kanyasu alisema kinachompa matumaini ya Mpango huo kupata mafanikio makubwa ni hatua ya Mawaziri kuanza kuiga mtindo wa uchapaji kazi wa Rais Magufuli akisema hatua hiyo itaharakisha sana katika kutatua matatizo mengi ya wananchi masikini, lakini pia akaeleza kuridhishwa na nidhamu katika ulipaji wa kodi hivi sasa.
Mbunge wa Mkuranga, Abdalah Ulega (CCM) alisema ili mpango huo uweze kufanikiwa na kuifanya nchi kuelekea katika uchumi wa viwanda utakaoivusha kirahisi kuelekea uchumi wa kati, suala la kutengwa maeneo maalumu ya viwanda halikwepeki, akisema hatua hiyo pamoja na mambo mengine itahuisha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF) aliitaka serikali kuelekeza macho yake katika kuendeleza Ukanda wa Mtwara akisema ukanda huo una utajiri usiopimika na ambao unaweza kuiondoa nchi katika umasikini uliopo.
Alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi ili kubaini ukweli wa kiwango cha deni la Taifa kutokana na kuwepo kwa taarifa zinazokinzana na kuongeza kwamba mataifa mengi yameporomoka kutokana na kushindwa kujua madeni yao ya taifa na namna ya kuyapatia ufumbuzi.
Alisema pamoja na kwamba Mpango unaelezea kukuza pato la Mtanzania kutoka Dola 1006 kwa mwaka kwenda 1,500, mkakati huo hautaweza kufanikiwa kwa kutupia macho sekta ya viwanda peke yake na badala yake maeneo ya kilimo, uvuvi, rasilimali za Mtwara kama gesi na pia ufufuaji wa Shirika la Ndege (ATCL) yatiliwe mkazo.
Habari leo

No comments:

Post a Comment