Sunday, 24 April 2016

Magazetini:Tanzania yaungana na dunia makubaliano tabianchi


TANZANIA ni miongoni mwa nchi wanachama 175 wa Umoja wa Mataifa zilizosaini Makubaliano ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Paris, yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika Ufaransa Desemba mwaka jana.

Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ndiye aliyepewa dhamana ya kutia sahihi makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika hafla ya kihistoria na ya aina yake iliyofanyika juzi Ijumaa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema haijawahi kutokea Mkataba au Makubaliano ya Kimataifa kutiwa sahihi na mataifa mengi katika siku ya kwanza kama ilivyokuwa kwa Makubaliano ya Paris.
Mataifa makubwa na ambayo yanachangia katika utoaji wa gesi chafu ya ukaa ikiwemo Marekani, China, Urusi, India, Ufaransa na mengineyo nayo yameweka sahihi zao.
Aidha, mtoto Gertrude Clement (16) kutoka Mwanza -Tanzania alizungumza katika hafla hiyo akiwakilisha ujumbe kutoka kwa vijana wenzie duniani kote.
Gertrude alizungumza kwa umahiri wa hali ya juu, akiainisha mambo kadhaa ambayo vijana wa kizazi chake na kijacho wangependa kuona kizazi cha sasa kikiyatekeleza kupitia makubaliano hayo ya Paris, ili nao waje kuishi na kuifaidi sayari ya dunia.

Na Habari leo

No comments:

Post a Comment