Monday, 25 April 2016

Milioni 43 zatafunwa watumishi hewa Kilimanjaro msako waendelea




Serikali mkoani Kilimanjaro imeendelea na operesheni ya kusaka watumishi hewa katika wilaya ya Same ambapo imebaini
watumishi hewa tisa ambao wameiingizia serikali hasara zaidi ya shilingi milioni 43. Saba kati ya watumishi hewa hao ni wale ambao  hawakuwepo katika vituo vyao vya kazi na wawili walikuwa wakiendelea kuchukuwa mshahara wakati walishastaafu kazi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya  habari akiwa wilayani Same, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadiki amewataja watumishi hao akiwemo Nestori Sebastian aliyekuwa akichukuwa mshahara ,kwa jina la  marehemu mama yake, aitwae Agripina Mbwambo.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa wa Kilimanjaro amesema  katika zoezi hilo wamebaini watumishi watatu waliyokwenda masomoni bila idhini ya mwajiri wao kinyume cha sheria ya utumishi hivyo inawafanya wahesabiwe kuwa hawapo kazini ambao wamesababishia serikali hasara zaidi ya milioni 4.5.
Katika taarifa hiyo mkuu wa mkoa amewataja watumishi wengine wawili ambao walipewa ruhusa ya kwenda masomoni lakini wakajiongezea muda bila idhini ya mwajiri wao huku wakiendelea kuchukuwa mshahara kinyume na utaratibu ,ambapo tayari wameshachukuwa zaidi ya shilingi milioni 31.

No comments:

Post a Comment