MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa hadhari ya kunyesha
kwa mvua kubwa kuanzia kesho hadi mwisho wa mwezi huu, itakayosabaishwa
na kimbunga kiitwacho Fantala.
Kimbunga hicho kipo katika eneo la Bahari ya Hindi kikienda kwa
mwendo wa pole pole na kilikuwa hakijaleta madhara, lakini kwa sasa
athari zake zimeanza kuonekana.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk
Agnes Kijazi alisema wanatarajia kuanzia kesho hali ya mvua itaendelea
kuongezeka katika maeneo ya Ziwa Victoria na maeneo ya Magharibi.
Alisema kutokana na upepo kuvutwa na kimbunga hicho kwenda baharini,
eneo kubwa la nchi litakuwa na mvua kubwa hivyo, wananchi wametakiwa
kuchukua hadhari “Sasa tuko katika msimu wa mvua za masika, lakini
kimbunga hiki kitasababisha ongezeko la mvua, hivyo ni vizuri tahadhari
zikachukuliwa,” alisema.
Alisema tatizo kubwa la kimbunga hicho ni mgandamizo mdogo wa hewa
unaoweza kuvuta upepo kutoka maeneo mbalimbali kwenda sehemu ambazo
kimbunga kipo. Dk Kijazi aliongeza kuwa, kila siku wakati wa kutoa
utabiri, watatoa tahadhari ya maeneo yatakayoathirika zaidi hivyo
wananchi wanapaswa kuzingatia utabiri wa kila siku.
Alisema vimbunga vimekuwa vikipewa majina na nchi zilizo Ukanda wa
Pwani ambayo hupendekeza kwa kufuata mpangilio wa herufi kulingana na
msimu unaoanza Novemba mpaka Aprili na hiki ni kimbunga ni cha sita,
lakini siyo vyote vyenye madhara kwa nchi.
Alisema vingine havijasikika kutokana na kutokuwa na madhara kwa
nchi, lakini Fantala kina madhara ya kusababisha kuongezeka kwa mvua
katika maeneo mengi ya nchi.
“Mpaka sasa tupo kwenye msimu wa mvua za masika zinazoendelea
kunyesha na kuna dalili zinazoonesha kimbunga hicho kimeanza kuleta
athari lakini kuanzia Jumapili na mvua zitaongezeka zaidi,” alisisitiza.
Saturday, 23 April 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment