JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman, amesema Sheria ya Mitandao ilitungwa na kupitishwa kwa lengo jema la kumlinda mtumiaji, jamii na usalama wa taifa la Tanzania.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu baadhi ya maswali ya Watanzania waishio Uingereza, kwenye mkutano uliofanyika katika Ubalozi wa Tanzania.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa, Jaji Mkuu alisema katika mkutano huo kuwa sheria hiyo ilitungwa kwa misingi mikuu mitatu, aliyoitaja kuwa ni kumpa mtumiaji uhuru wa kutoa maoni au taarifa, mtu kuwa na faragha na kulinda usalama wa taifa.
Hata hivyo, Jaji Mkuu alisisitiza kuwa uhuru huo unalindwa kikatiba, lakini ni lazima uwe na mipaka kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 30(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Sheria hii inakupa uhuru wa kutumia mtandao kumlinda mwanajamii wenzako”. “Hapa Uingereza nimezungumza na Mwendesha Mashtaka Mkuu ambaye aliniambia kuwa asilimia 60 ya makosa yanafanyika chini ya sheria ya makosa ya kujamiiana yanatokana na mitandao,” alisema Jaji Mkuu wakati akijibu swali kuhusu sheria ya makosa ya mitandao alipoulizwa katika mkutano huo wa Watanzania.
Akifafanua zaidi, Jaji Mkuu alisema, watu watatu kati ya wanne nchini Tanzania wakiwemo watoto, wanamiliki simu za mkononi ambayo ni sawa na watu milioni 35 kati ya milioni 45.
Alisema, hali hiyo inapaswa kuwa na uhuru na udhibiti wa matumizi, hivyo kusisitiza kuwa, sheria hiyo imetungwa kwa nia njema.
Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015 imekuwa ikielezwa kuwa na manufaa makubwa ya kudhibiti makosa ya mitandaoni hasa kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii nchini, kumlinda mtumiaji na kuhakikisha usalama wa nchi.
Sheria hiyo imekuwa ikitoa adhabu kwa mtumaji wa taarifa, picha au ujumbe hatarishi pamoja na mtu anayeupokea na kuusambaza.
No comments:
Post a Comment