Monday 16 May 2016

Waziri mkuu Majaliwa azungumzia mpango wa serikali kuhusu waliojilipa mishahara hewa nchini.

 
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kuanza kazi kwa kupambana na wala rushwa kurejesha umoja, ili rasilimali zilizopo ziwanufaishe Watanzania wote.

Alisema katika mapambano hayo, wanalenga pia kushughulika na waliosababisha uwapo wa watumishi hewa baada ya kumaliza kuwabaini watumishi hao kote nchini.

“Jambo tuliloamua kuanza nalo ni kupambana na rushwa. Tumeamua kufanya hivyo kurudisha umoja na maelewano miongoni mwa Watanzania, tunataka tuibadili Tanzania iwe ni ya Watanzania wote… tumechoka kuambiwa sehemu fulani mradi umekamilika halafu ukienda kuangalia hukuti kitu na fedha ile haipo,” alisema na kushangiliwa na Watanzania waishio Uingereza.

Majaliwa alizungumza na Watanzania hao juzi kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini London, Uingereza. Waziri Mkuu alikuwa nchini humo akimwakilisha Rais John Magufuli kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuhudhuria mkutano wa kujadili namna ya kupambana na rushwa.

Alisema, Tanzania ina rasilimali nyingi na manufaa ya rasilimali hizo hayapaswi kuwa neema kwa wachache bali wananchi wote.
Akizungumzia suala la kusaka watumishi hewa, Majaliwa alisema Serikali itawashughulikia wale wote waliohusika katika hilo.

“Wafanyakazi hewa wamefikia zaidi ya 10,000 na tumeokoa zaidi ya Sh bilioni 4.5 zilizokuwa zikipotea kila mwezi. Tukikamilisha kusaka watumishi hewa, sasa tutataka kujua ni akina nani walikuwa wakipokea fedha hizo. Waliohusika tutashughulika nao,” alisisitiza.

Alisema hivi sasa Serikali inalenga kuwa na watumishi wanaofanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na uwajibikaji mahali pa kazi.

“Hiki ndicho kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano na suala hili litakuwa endelevu”, alisema Majaliwa. Uchumi na viwanda Akizungumzia kuhusu ukuaji wa uchumi, Waziri Mkuu alisema, lengo la Serikali hivi sasa ni kuona kuna ukuaji wa uchumi unaoenda sambamba na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Majaliwa alisema, viwanda vingi viliuzwa na watu waliovinunua wakageuza kuwa ni maghala ya kufugia wanyama.

“Sisi tunataka vifufuliwe ili teknolojia mpya na za kisasa zije Tanzania. Nafasi ya kuwekeza iko kwa Watanzania wote walioko nyumbani na ninyi mlioko nje,” alisema.

Alisema, ardhi ipo ya kutosha na akawataka wawaalike marafiki zao kuwekeza nchini, ili mradi wawe ni watu makini, wenye nia ya dhati ya kuwekeza kwa mitaji na si madalali.

Alisema Serikali inataka usindikaji wa mazao na bidhaa ufanyike nchini badala ya kupeleka mazao ghafi nje ya nchi. Alisema kwa njia hiyo Tanzania itakuwa imezalisha ajira kwa wananchi wake.

“Kuna Watanzania wanaishi Botswana, Ujerumani na Poland wameshaleta wawekezaji nchini. Kwa mfano wa Poland wameleta mradi wa umeme katika vijiji vitano wilayani Ileje. Kwa hiyo ninyi endeleeni kuishi Uingereza lakini mhakikishe kuwa ukaaji wenu hapa unaleta tija kule nyumbani. Kumbukeni Tanzania na muwe tayari kuihudumia Tanzania,” alisema.

No comments:

Post a Comment