Thursday, 26 May 2016

Hii ndio kauli ya Rais Magufuli kwa Makandarasi nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli, amewataka makandarasi
wasikubali kutoa rushwa na kuwafichua watendaji wanaowaomba rushwa ili kuwapatia fursa katika miradi ya ujenzi, kwa kuwaripoti katika taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Rais Magufuli ameyasema hayo katika mkutano wa mashauriano na maonyesho wa mwaka wa makandarasi nchini, ambapo amesema sekta hiyo ya ujenzi inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya rushwa ambayo huongezwa katika orodha ya gharama halisi ya ujenzi kwaajili ya watendaji wa serikali ambao hudai ili kutoa upendeleo.

Rais John Magufuli alitumia muda huo kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya watendaji wabovu ambapo amesema kwa wanaofikiri vita yake dhidi yao ni ya muda, wanajidanganya.

Katika upande mwingine Rais Magufuli pia amewaasa makandarasi kuhakikisha wanajadili na kujipanga kupata kazi katika miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta litakalojengwa kutoka Uganda mpaka Tanzania, kwa lengo la kutumia fursa zitolewazo na miradi hiyo la sivyo makandarasi wa Tanzania watabaki kuwa wasindikizaji.

Kwa upande wake waziri wa Ujenzi, mawasiliano na uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema tayari serikali imeanza kulipa madeni ya makandarasi tangu Julai 2015 na kusisitiza makandarasi wazalendo kupewa fursa katika miradi endapo watakidhi vigezo husika na kukamilisha kazi kwa viwango vyenye ubora.

Mkutano huo wa SIKU MBILI wa mwaka wa bodi ya usajili wa makandarasi (CRB) uliobeba kauli mbiu ya “juhudi za makusudi za kuwaendeleza makandarasi wazalendo kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi; changamoto na namna ya kuzitatua”, uliambatana na maonesho ya zana mbalimbali za ujenzi ulihudhuriwa na makandarasi, washauri na wadau wa sekta ya ujenzi ambapo Rais alipata fursa ya kutoa vyeti kwa wadhamini na wageni kutoka nje ya nchi

No comments:

Post a Comment