Sunday, 15 May 2016

Lady Jay Dee kutoa maamuzi haya baada ya aliyekuwa mme wake Gardner kumzalilisha.

 
Siku 14 tangu Mtangazaji wa Clouds Fm Gardner Habash kudaiwa kutoa lugha ya udhalilishaji dhidi ya aliyekuwa mke wake Judith Wambura, mwanamuziki huyo maarufu kwa jina la Lady Jaydee, amesema kesho anatarajia kutoa tamko rasmi kuhusu suala hilo.


“Nipo katika maandalizi ya tamasha langu ndiyo maana ilikuwa vigumu kwangu kulizungumzia hili, Jumatatu nitatoa tamko,” alisema Jaydee.

Mei 13 kupitia mwanasheria wake Amani Tenga kutoka kampuni ya Law Associates Advocate, alimwandikia barua ya kumtaka mtangazaji wa Clouds Fm, Gardner Habash kuomba radhi mbele ya umma ndani ya siku 7 kwa kauli ya udhalilishaji aliyoitoa dhidi yake.

Gardner  anadaiwa kutamka maneno ya udhalilishaji dhidi ya Jaydee Mei 6 mwaka huu na kurekodiwa kisha video kusambazwa katika mitandao ya kijamii, katika ukumbi wa CDS PARK (zamani TCC) alipokuwa akisherehesha tamasha la Miss TIA 2016, 

Taarifa iliyosomeka katika barua hiyo ya mwanasheria ilimtaka Gardner aombe radhi na iwapo akikaidi, akishindwa au kuzembea ndani ya siku saba, atachukuliwa hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kesi ya udhalilishaji na kashfa.

Mwananchi lilimtafuta Gardner na kumuuliza iwapo amepokea barua hiyo na matarajio yake ya kujibu tuhuma zinazomkabili, lakini mtangazaji huyo alikaa kimya kwa muda wa sekunde 10 na baadaye alisema; “sina maoni yoyote kuhusu jambo hili.”

Barua iliyoandikwa na mwanasheria huyo ilisomeka kuwa kauli ya Gardner, maneno yake hayo yalikuwa yanamhusu Jaydee moja kwa moja hivyo kusababisha udhalilishaji mbele ya umma.
“Kutokana na udhalilishaji huo, mteja wetu ameathirika kwa namna nyingi, moja ikiwa ni kumletea sifa mbaya kama mwanamke mbele ya umma, kuhatarisha shughuli zake za kibiashara za kila siku ambazo ni muziki na burudani,” kilieleza kipengere cha tatu cha barua hiyo.

Kipengere cha nne kilieleza, “mteja wetu ameumia kisaikolojia na baadhi ya maslahi yake yameathirika kwa kiasi kikubwa sana, ukizingatia maneno hayo yameendelea kusambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.”

Mwanasheria huyo alisema iwapo wawili hao walishapeana talaka chini ya sheria za ndoa za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inakataza mtu kuongelea jambo lolote linalo husiana na mambo ya ndoa.

Aidha barua hiyo ilimkanya Gardner kuhakikisha anakamilisha utaratibu aliopewa kwa wakati, na iwapo akishindwa kutekeleza agizo hilo, itamlazimu kulipia gharama za usumbufu katika hatua za kisheria zitakazochukuliwa. 

Ilielezwa kuwa wadhamini na waandaaji wote wa tamasha la Miss TIA 2016, wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria pia kutokana na tamasha hilo kutumika kumkejeli na kumdhalilisha mwanamuziki huyo.

Kwa muda wa wiki moja tangu mtangazaji huyo atoe hauli yake, Lady Jaydee aliyesaini mkataba chini ya lebo ya Rockstar4000 amekuwa kimya licha ya watu mbalimbali kujitokeza na kumtaka Gardner aombe radhi.

Mkurugenzi wa Rockstar4000, Seven Mosha alizungumza na gazeti hili na kusema kwamba mpaka sasa bado wanaendelea kufuatilia barua hiyo na kwamba angetoa jibu baadaye, “Ladyjaydee atazungumza na umma siku ya Jumatatu.”

Siku moja baada ya mtangazaji huyo kutoa kauli hiyo hadharani, Naibu wa Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla alisema kitendo hicho ni udhalilishaji si tu kwa mwanamuziki huyo bali ametukana wanawake wote.

“Nikiwa balozi wa wanawake natoa rai kwa uongozi wa Clouds fm kumtaka Gardner afute kauli yake  na aombe radhi kwa Jaydee na kwa umma ili kulinda heshima yao,” aliandika Kigwangalla kupitia ukurasa wake wa twitter

Na Mwananchi

No comments:

Post a Comment