BENKI ya Dunia (WB) imeahidi kutoa Dola za Marekani milioni nne sawa na zaidi ya Sh bilioni nane kwa ajili ya ruzuku katika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mara baada ya kumaliza kikao na watendaji wakuu wa Benki ya Dunia wanaosimamia miradi ya sekta ya madini. Alisema sehemu ya fedha hizo za ruzuku ambayo ni ya awamu ya tatu zitatolewa Septemba mwaka huu.
Alisema fedha hizo zitatumika kufadhili uendelezaji wa vituo saba vya mfano vya utafutaji na uchimbaji mdogo wa madini ambavyo vitachaguliwa na wizara baada ya kufanya tathmini ya maeneo yanayoweza kuwekwa vituo hivyo.
“Sio hivyo tu, fedha hizi za Benki ya Dunia zinalenga kuwafadhili wanawake kwenye shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, ukataji na uchongaji wa madini ya vito ili idadi ya wanawake wanaojishughulisha na sekta ya madini iongezeke,” alisema Profesa Muhongo.
Aidha, alitoa mwito kwa wataalamu wote wanaosimamia miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia katika sekta ya Madini kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo uende kwa kasi ili kuleta matokeo yaliyotarajiwa.
Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeendelea kutoa ruzuku katika uchimbaji madini mdogo, na katika mwaka wa fedha 2015/16 zilitengwa takribani Sh bilioni 7.2 ambazo zilitolewa kwa vikundi 111 vya wachimbaji wadogo na watoa huduma mbalimbali katika sekta ya uchimbaji madini mdogo.
Vilevile, katika mwaka wa fedha 2013/2014, fedha za ruzuku zilizotolewa kwa wachimbaji wadogo zilikuwa ni Dola za Marekani 500,000 sawa na takribani Sh bilioni moja zilizotolewa kwa waombaji 11. Fedha hizi ziliwalenga wachimbaji madini wadogo pekee tofauti na awamu zilizofuata.
Utoaji huo wa ruzuku unaenda sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini waliopata ruzuku husika ili kuhakikisha kuwa shughuli zilizopata ufadhili zinaleta tija.
Na Habari leo
No comments:
Post a Comment