Thursday 5 May 2016

Mgazetini:Sakata la bei ya sukari laibuka tena bungeni


SAKATA la kupanda kwa bei ya sukari limeibuka tena bungeni na safari hii Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) ameomba mwongozo wa kutaka Kikao cha Bunge kiahirishwe ili kujadili suala hilo la dharura.

Akitumia kifungu cha Kanuni za Bunge cha 47(1, 2, 3), mbunge huyo alisema bungeni mjini hapa jana, kuwa suala hilo ni muhimu kwa Watanzania hivyo ni vyema likajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Alisema tangu itangazwe utaratibu wa kusitisha sukari kuingizwa nchini kutoka nje, bidhaa hiyo imekuwa adimu na bei yake imekuwa inapanda kila siku na kusababisha maisha ya wananchi kuzidi kuwa magumu.

Hata hivyo, kabla ya kumaliza kuwasilisha hoja yake hiyo, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimkatisha na kubainisha kuwa hoja hiyo si dharura, lakini pia tayari ilishatolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu akijibu hoja iliyoibuliwa bungeni hapo inayohusu pia bei ya sukari, Waziri Mkuu alisema serikali imeruhusu kiasi kidogo cha sukari kuingizwa nchini ili kupunguza tatizo la upungufu wa bidhaa hiyo.

Kwa mujibu wa Majaliwa, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari kwa mwaka wakati nchi inahitaji tani 420,000 hivyo kuwepo na upungufu wa tani 120,000.

Aidha, mapema mwezi uliopita, serikali ilitangaza kuwa bei elekezi ya sukari itakuwa Sh 1,800 kwa kilo, lakini hali katika maeneo mbalimbali nchini ni tofauti, kwani bidhaa hiyo muhimu inauzwa kwa bei ya juu.

Katika maeneo mbalimbali ukiwamo Mkoa wa Dar es Salaam, sukari inauzwa kuanzia Sh 2,200 hadi Sh 2,500 kwa kilo, wakati baadhi ya mikoa ikiwamo Kagera ambako inazalishwa katika Kiwanda cha Kagera kilichopo Missenyi, bei inatajwa kufikia hadi Sh 25,000 kwa kilo moja.

Baadhi ya wafanyabiashara nchini wameamua kufanya njama za kuficha bidhaa hiyo ili kuonekana kuwa kuna uhaba ili waruhusiwe kuagiza kutoka nje, jambo ambalo limekwishakataliwa na Rais John Magufuli.

Wiki iliyopita, mkoani Singida, wananchi walisaidia kukamatwa kwa mifuko 655 ya sukari sawa na tani 24.3, na kutiwa nguvuni wafanyabiashara wawili pia wakihusishwa na bidhaa hiyo ambayo ilifichwa stoo
.
Waliokamatwa ni Mohamed Alute Ally (44) mfanyabiashara wa Unyankindi aliyekutwa na mifuko 335 ya kilo 25 kila mmoja na Yusufu Suleiman (39) mfanyabiashara wa Minga aliyepatikana na mifuko 320 ya kilo 50.

Taarifa ya kukamatwa kwa sukari hiyo na wafanyabiashara hao ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Amanzi.
Taarifa zilieleza kuwa mfuko mmoja wa sukari ambao huuzwa kwa Sh 92,650 sasa unauzwa kati ya Sh 115,000 na Sh 120,000 huku kilo moja ikiuzwa kati ya Sh 2,400 na 2,800 kwa kilo kinyume cha bei elekezi ya Sh 1,800.

Gazeti hili lilifanya jitihada za kuwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Henry Simwanza kuzungumzia hali ya bei hiyo jana, lakini awali alipopigiwa simu alieleza kuwa yuko bungeni, lakini baadaye hakupokea simu ya gazeti hili kutwa nzima alipotafutwa.

Na Habari leo

No comments:

Post a Comment