MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Uchumi, Dk Haji Semboja, ameshauri bei elekezi ya sukari itazamwe kwa kuzingatia sera na sheria za nchi za uwekezaji, ili isiwanyonye walaji, lakini pia isiwafukuze wawekezaji.
Ametaka bei hiyo elekezi, iwe itakayosaidia wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha sukari kuja kwa wingi nchini na kuzalisha sukari ya kuuza ndani na nje ya nchi na wakulima wa miwa wapate soko zuri la malighafi hiyo. Alitoa ushauri huo kwenye kipindi cha Kipima Joto, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV juzi usiku na kufafanua kuwa suala la sukari, linaweza kutazamwa kwa pande tatu ambazo ni kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Kijamii Alisema sukari ni kawaida kutazamwa kijamii, wakati wa msimu wa kufunga uzalishaji viwandani unapowadia. “Katika nyakati hizi mahitaji huwa makubwa kwa sababu pia ya hofu ya wananchi ambao huogopa bei itapanda, hivyo kama mwananchi alikuwa na kawaida ya kununua kilo mbili au tatu, atanunua hata kilo tano na kusababisha ongezeko la mahitaji linalochangia kuongezeka kwa uhaba,” alisema Dk Semboja.
Kiuchumi Katika mtazamo wa kiuchumi, Dk Semboja alisema bei inapokuwa kubwa, wakulima wa zao la miwa nchini hupata faida kwa kuwa wao ndio wanaouza malighafi za sukari, hivyo bei ya miwa huongezeka na hilo ni jambo zuri kwao. Mbali na wakulima wa miwa kunufaika, msomi huyo wa uchumi alisema hata wawekezaji wanaovutiwa kuwekeza mitaji yao katika sekta hiyo, huongezeka ndio maana kuna umuhimu wa kuhakikisha bei elekezi haimuumizi mlaji, lakini pia haifukuzi wawekezaji.
Alishauri bei elekezi ya sukari, iangaliwe kwa umakini kwa kuhusisha wadau wote wa sukari, wakiwemo wakulima wadogo na wakubwa, kama ambavyo wadau wa nishati na maji wanavyofanya kupitia Mwamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura). “Hapa nchini kuna Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), ndiyo inapaswa kuhakikisha tija, wao walipaswa kuwaita wadau wajadili na kuja na bei elekezi ambayo haitamgandamiza mlaji na wahakikishe bidhaa hiyo inapatikana,” alisema Dk Semboja.
Changamoto Alisema katika uchumi bei inaposhushwa sana, inakinzana na sera za uwekezaji, jambo linaloweza kusababisha nchi kuwa hatarini kukosa wawekezaji katika uzalishaji wa sukari, huku waliopo wakishindwa kuwalipa wakulima wadogo, ambao huuza malighafi zao kwenye viwanda hivyo. Aliongeza kuwa kama soko la sukari litakuwa halieleweki linatawaliwa na nguvu ipi; kati ya nguvu ya soko ambayo ni ya kiuchumi au nguvu ya Serikali, ni vigumu kwa wawekezaji kuja kuwekeza.
Alionya kuwa jambo hilo haliwezi kumaliza tatizo la uhaba wa sukari nchini, kwa kuwa kwa sasa viwanda vilivyopo vinazalisha chini ya kiwango cha mahitaji kwa mwaka. Alisema takwimu za sasa zinaonesha kuwa mahitaji ya sukari nchini na ile ya viwandani kwa mwaka ni tani 420,000, lakini viwanda vilivyopo huzalisha tani 300,000, hivyo kila mwaka kuna upungufu wa tani 120,000.
Alisema kama kuna wafanyabiashara walinunua sukari kwa bei kubwa kabla ya bei elekezi kutajwa, wakiuza kwa bei elekezi watapata hasara na huenda hiyo ikawa moja ya sababu ya wao kuhodhi sukari, ili kusubiri bei itengamae na wao wauze bila kupata hasara. “Lakini kwa upande mwingine wanaweza kuuza, ila wanapomaliza hawaendi tena kununua sukari kwa sababu inauzwa kwa bei tofauti, watashindwa kurudisha fedha waliyonunulia, huenda ndio maana wengine wanaghairi na kuacha kuuza,” alisema Dk Semboja.
Alisisitiza suluhu pekee ni kutazama sera na sheria za nchi kwenye uwekezaji, ili zisaidie wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha sukari waje kwa wingi, ili kuzalisha sukari na kuiuza hata nje ya nchi na wakulima wa miwa wapate soko la malighafi hiyo. Profesa Lipumba Wakati huo huo, Taasisi ya Ushauri wa Masuala ya Habari (CZI), imeelezea kusikitishwa na kauli ya mwanasiasa mkongwe, Profesa Ibrahimu Lipumba, kuhusu suala la sukari na kumtaka mwanasiasa huyo awe mkweli, kuwaeleza Watanzania namna hali ya sukari ilivyo nchini.
Taarifa ya Ofisa Habari na Uhusiano wa CZI, Gaudency Tungaraza, iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilimtaka Lipumba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF kabla ya kujitoa, awaeleze Watanzania ukweli kuhusu hujuma iliyofanywa na wafanyabiashara wa sukari kwa wananchi. Tungaraza katika taarifa yake amesema kauli ya Lipumba, haina mashiko na kushauri
wananchi waidharau, kwa kuwa chanzo cha uhaba wa sukari ni wafanyabiashara wasio waaminifu na waliokuwa wanakwepa kodi na vita hiyo waliipanga muda mrefu na baada ya mipango yao kujulikana, wakaanza mapambano kuhakikisha Serikali inakwama.
“CZI tunaamini kwamba Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli ana nia njema na Watanzania wenzake ; na anajua namna Watanzania hao walivyoumia kwa miaka mingi, lakini wakati anajaribu kuweka mambo sawa ili wananchi wa kawaida nao watumie rasilimali za nchi yao vizuri, kundi la watu waliozoea kula bila kuulizwa wanakwamisha juhudi za Rais ambazo anazifanya kwa matakwa ya wananchi wake,” alisema Tungaraza katika taarifa hiyo.
Profesa Lipumba alinukuliwa na vyombo vya habari juzi na jana, akidai kuwa Rais Magufuli ndiye chanzo cha kuadimika kwa bidhaa hiyo, baada ya kutangaza kusitisha uingizwaji wake kutoka nje ya nchi. “Rais Magufuli anasemaje sukari isiagizwe kutoka nje ya nchi wakati anajua iliyopo haitoshi… mimi naona yeye ndiye aliyesababisha uhaba wa sukari,” alidai Profesa Lipumba, alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CUF, zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam
Na Habari leo.
No comments:
Post a Comment