Friday 13 May 2016

Waziri mkuu Majaliwa azungumza haya kuhusu mkutano mkutano wa kimataifa wa kupambana na rushwa nchini London.

 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wakuu wa nchini na washiriki wa mkutano wa kimataifa wa kupambana na rushwa wamevutiwa na jitihada ambazo Tanzania imezichukua kukabiliana na janga hilo.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ushiriki wake kwenye mkutano wa siku moja wa Wakuu wa Nchi ulioitishwa kujadili suala la kupambana na rushwa duniani uliofanyika Lancaster House, jijini London, Uingereza.

Waziri Mkuu Majaliwa katika kikao cha kwanza kilichohudhuriwa na wakuu wa nchi na viongozi wa kitaifa wapatao 20, ameelezea jinsi Tanzania ilivyoweza kupambana na rushwa kwa kuzingatia .

vigezo vikuu vinne, ambavyo ni kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria zinazohusu masuala ya rushwa; uanzishwaji wa mahakama maalum ya mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi Julai, mwaka huu; mikakati ya udhibiti wa fedha za miradi ya wananchi na utaratibu wa kubaini wala rushwa kwa kushirikisha jamii ikiwemo kutunza siri za watoa taarifa.

Waziri Mkuu alisema alipata fursa ya kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. David Cameron ambaye mbali na kupongeza juhudi za Serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kupambana na rushwa pia aliahidi kutoa mwaliko ili Tanzania iweze kushiriki kwenye mkutano mwingine wa masuala ya rushwa utakaofanyika Japan, Julai mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ofisi yake haijahusika na kuandaa mkutano wa wanadiaspora waishio Uingereza kama ambavyo imedaiwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna watu maalum wamechaguliwa kushiriki mkutano huo.

Amesema mkutano huo umepangwa kufanyika kesho na uko wazi kwa Watanzania wote kushiriki ili waje kusikiliza nchi yao imefanya nini na kama kuna masuala yanahitaji ufafanuzi, watapatiwa fursa hiyo.

No comments:

Post a Comment