Sunday 15 May 2016

Waziri Nape awajibu wanaotaka Bunge liwe ‘live’ kwa kauli hii.

 
SERIKALI imetoa ufafanuzi kuwa kuanzishwa kwa studio inayoratibu matangazo ya vikao vya Bunge, vinavyoendelea mjini Dodoma, ni uamuzi uliopitishwa na wabunge wenyewe na hauna mkono wa Serikali, kama inavyodhaniwa na watu wengi.


“Uamuzi wa kuanzisha studio ya Bunge si wa Nape wala Serikali, ulipitishwa na Bunge wakati Nape wala Serikali ya Awamu ya Tano, haijaingia madarakani, walipitisha na bajeti, Kanuni ndo zikasema chombo cha utangazaji kitatangaza mikutano ya Bunge kwa utaratibu na mipango ya Bunge, sasa kuingizwa Serikali kunatoka wapi?” Alihoji.

Alisema Serikali kama wasimamizi wa habari, wapo tayari kusimama kati ya Bunge na wadau wa habari, kuzungumzia upungufu uliopo, ili kupatia ufumbuzi kuhusu studio hiyo na kutorushwa kwa vikao vya Bunge moja kwa moja kama ilivyokuwa zamani.

“Wadau wa habari hata Jukwaa la Wahariri (TEF), limekuja kutembelea studio hiyo ya Bunge…mlikaa wenyewe wabunge mkapanga kuanzishwa kwa studio hii na taratibu zake sio sisi Serikali, tafadhali twendeni taratibu, tusibebeshane mzigo,” alisema.

Aliwataka wabunge kutenda haki na kuacha kusema Tanzania hakuna uhuru wa habari, wakati ripoti ya Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka, imeonesha katika nchi 180, Tanzania ni ya 11 yenye uhuru wa habari na kwa Afrika Mashariki ni ya kwanza kwa uhuru wa habari.

Akizungumzia madai ya Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), aliyedai vikao vya Bunge vinaoneshwa TBC saa 3:00 za usiku watu wakiwa wamelala na kudai kuwa Nape amewadanganya Watanzania kusema vikao hivyo vinaoneshwa baada ya taarifa ya habari, alisema TBC ni uamuzi wao wenyewe kuonesha muda huo.

“Vituo vingine vinaonyesha muda ambao ni mwisho wa studio ya Bunge ambao ni saa 3:00 usiku. Studio ya Bunge huwa inachelewa saa moja na huu ni utaratibu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola,” alisema.

Alisema katika Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari, wameweka haki zote za wanahabari na utaeleza elimu anayopaswa kuwa nayo mwanahabari ili kuondokana na ‘makanjanja’.
Mchakato wa utungaji wa sheria hiyo utakamilika hivi karibuni, hivyo kuanza kutumika. 

Akizungumzia ushauri wa wabunge wa kuanzishwa kodi maalumu kwenye ving’amuzi kwa ajili ya kuendeshea TBC, ili iachane na ruzuku ya Serikali na fedha za matangazo, alisema suala hilo wameshalijadili ngazi ya Wizara na kwa sasa lipo ngazi ya Wizara ya Fedha na likikubaliwa, litapelekwa bungeni ili kuanza utekelezaji.

No comments:

Post a Comment