Friday 24 June 2016

Haya ndio yaliobainika katika utafiti mpya uliofanywa kuhusu utendaji kazi wa Rais Magufuli.


Utafiti uliofanywa na Taasisi Huru ya Kijamii ya CZI katika mikoa 15 nchini kuhusu utendaji kazi wa Rais John Magufuli, umebaini kuwa rais anakubalika kwa wananchi kwa asilimia 89 tangu aingie madarakani.


Hayo yamo kwenye taarifa ya matokeo ya utafiti uliofanywa Tanzania Bara na Visiwani, kuangalia utendaji kazi wa rais kwa miezi minane tangu aingie madarakani; anaripoti Ikunda Eric.

Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, jopo la watafiti hao likiongozwa na mwanadiplomasia kijana Dotto Nyirenda, walisema walihoji makundi matatu ya watu.

Nyirenda alisema kwa ujumla rais anakubalika kwenye jamii kwa asilimia 89 na hiyo inatokana na majibu ya utafiti huo kutoka makundi matatu yaliyohojiwa. Kundi la kwanza lililohojiwa ni vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 18 ambalo lilisema wanaamini Rais Magufuli ataleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kurejesha nidhamu ya masomo shuleni.

Nyirenda alisema kundi hilo linaamini kwa asilimia 78 utendaji kazi wa Rais Magufuli na kwamba ataleta mageuzi kwenye elimu, ikiwa ni pamoja na kuondoa tatizo la madawati, mitaala na kurudisha nidhamu ya walimu.

Hata hivyo, katika kundi hilo asilimia 22 wanaona huenda rais asifanikiwe kwenye sekta ya elimu na pia kuondolewa kwa michezo shuleni kutadidimiza maendeleo ya michezo nchini.

Kundi la pili lililohojiwa ni vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 30 wanaoamini utendaji kazi wa rais kwa asilimia 82, na kwamba ataleta mabadiliko kwenye sekta ya ajira na elimu kwa sababu amelivalia njuga tatizo la watumishi hewa na ajira za kwa wahitimu zitapatikana kwa kiasi fulani tofauti na ilivyokuwepo tatizo la watumishi hewa.

Kundi la tatu ni wananchi wenye umri wa miaka 30 hadi 60 ambao asilimia 89 walisema upo uwezekano wa watumishi wa umma kurejesha imani kwa serikali kutokana na juhudi za rais alivyopambana na ufisadi na rushwa.

Pia kundi hilo linaamini kwa rais atamaliza matatizo ya wazee kwa kuanza kuwalipa posho kwa mwezi lakini pia wanaamini nidhamu ya watumishi wa umma itaongezeka. Mikoa iliyofanyiwa utafiti ni Tanga, Dodoma, Kusini Pemba, Kaskazini Unguja, Tabora, Kigoma, Simiyu, Morogoro, Pwani, Arusha, Manyara, Geita, Mara na Ruvuma.

No comments:

Post a Comment