Serikali imetoa siku mbili kwa mamlaka ya Bandari nchini TPA kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika mtambo wa
kupima mafuta (flow meter) ulioko Kigamboni jijini Dar es salaam ambapo miongoni mwa kasoro hizo ni pamoja na uharibifu wa kamera za ulinzi zinazodaiwa kuungua na kusababisha kukosekana kwa ulinzi wa uhakika wa mitambo hiyo kwenye eneo hilo.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea mitambo hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Leonard Chamuriho amesema kuwa Serikali haiko tayari kuona mradi uliojengwa kwa ajili ya kuboresha mapato ya malighafi ya bidhaa ya mafuta unatumika kinyume na matarajio yaliyokusudiwa na hivyo uharibifu uliojitokeza katika mitambo hiyo ni lazima urekebishwe haraka ili kuweka viwango bora vya utoaji huduma hiyo.
Aidha Katibu Mkuu huyo amesema kuwa mtambo huo ambao upo katika kipindi cha majaribio ukiwa na miezi miwili toka uanze umeonekana kuwa na mapungufu mbalimbali ya uharibifu ambapo mbali na kamera mbili za ulinzi kuungua pia vifaa mbalimbali vimeonekana kutofanya kazi zikiwemo valve za mitambo hiyo ambazo zinadaiwa kuharibiwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni na kusababisha utendaji kazi wa mitambo hiyo kupungua.
Pia imebainika kuwa mafuta yanayoingizwa nchini yanaingizwa na kupokelewa yakiwa machafu hali ambayo inaleta usumbufu katika kuyachuja katika mitambo hiyo huku akiwataka wahusika wa bandari kufuatilia uingizwaji wa mafuta machafu.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Mtambo wa Kupima Mafuta TPA Mhandisi Masry Mhayaya ameelezea namna uharibifu wa vifaa mbalimbali vya mtambo huo ulivyotokea huku akiahidi kushughulikia tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment