Thursday, 30 June 2016

Serikali yatenga kiasi hiki cha Fedha kwa ajili ya kukarabati Shule Kongwe nchini.


SERIKALI ya Awamu ya Tano imetenga Sh bilioni 33 kwa ajili ya mpango maalumu wa ukarabati mkubwa na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali, yakiwemo majengo ya madarasa, mabweni na nyumba za walimu katika shule kongwe za sekondari za serikali nchini.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa mpango huo katika Shule ya Sekondari ya Mzumbe iliyopo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Profesa Ndalichako alisema mpango huo wa miaka miwili utahusisha shule kongwe 88 za serikali kwa kufanyiwa ukarabati mkubwa wa miundombinu, majengo ya madarasa, nyumba za walimu, mabweni, majengo ya chakula na uboreshaji wa maabara na vitendea kazi vyake.

Waziri huyo alikuwa pia mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Elimu Tanzania iliyofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mzumbe na kuhudhuriwa na wadau wa sekta ya elimu wakiwemo wakuu wa shule za sekondari za serikali na maofisa elimu wa mikoa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

Alisema utekelezaji wa mpango huo unatarajia kuanza wakati wotote baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Serikali na kuanza kutumika na utaanza kwa awamu ya kwanza ambako shule kongwe 33 zitahusika.

“Tumekadiriwa kuwa kila shule itagharimu shilingi bilioni moja na kwa maana hiyo shule 33 zimeingizwa awamu ya kwanza. Fedha hiyo inaweza ikapungua kulingana na mazingira ya kitadhimini ya uchakavu wa majengo,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema uboreshaji wa elimu ni pamoja na ubora wa majengo na miundombinu mingine katika shule hizo, na lengo la kuzirejesha katika uhalisia wake wa zamani wa kuwa na mandhari nzuri za kuvutia wanafunzi, walimu na wazazi.

“Shule hizi tumeziweka katika mpango maalumu wa miaka miwili kukarabatiwa majengo yake, miundombinu ya kufundishia, vifaa vya kila somo, vitabu vya kufundishia na kujifunzia, vifaa vya kutosha vya maabara na kuboresha makazi ya walimu,” alifafanua Profesa Ndalichako.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais Tamisemi, Juma Kaponda, alimpongeza Waziri Ndalichako kwa kusimamia uboreshaji wa shule kongwe za sekondari na kuomba wadau mbalimbali waliosoma shule kongwe hizo na wanazo nyadhifa kubwa serikalini na sekta binafsi kuona wanao wajibu wa kuchangia maboresho hayo.


USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment