MAREKEBISHO ya Sheria mpya ya Manunuzi, yamewasilishwa bungeni yakitamka kufyeka posho za watendaji, wanaosimamia mchakato wa zabuni na kuondoa vikao vya bodi kutoka 12 kwa mwaka hadi vinne, ikisisitiza kuziba mianya ya rushwa na kuongeza uwazi.
Aidha, muswada wa marekebisho hayo, unataka kampuni au mshauri wa nje ili apewe zabuni katika shughuli zinazogharimiwa na fedha za umma, ahakikishe asilimia 60 ya wafanyakazi wa kampuni yake ni Watanzania.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, aliyasema hayo jana mjini Dodoma wakati akiwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2016.
Kupungua kwa vikao vya bodi, kumeelezwa na Dk Mpango kuwa kutapunguza gharama zinazotokana na posho ya vikao vya bodi ya zabuni na ada zinazolipwa kwa kamati zinazohusika na mchakato ya zabuni.
Aidha, posho zinazotokana na utekelezaji wa majukumu ya kazi ya kila siku ya washiriki itafutwa. Hata hivyo, imeruhusu kuwapo kwa vikao vya dharura pale Mwenyekiti wa Bodi akiona ni lazima.
Pamoja na kupunguzwa vikao, muda wa zabuni nao umepunguzwa na pia taasisi nunuzi itaruhusiwa kufanya majadiliano ya bei wakati wa mchakato wa zabuni kwa lengo la kupunguza bei ya ununuzi na kuongeza bei ya kuuza mali za serikali.
Dk Mpango alisema sheria hiyo mpya, itaziba mianya ya rushwa, kuongeza kasi, uwazi, uwajibikaji na kuleta upendeleo maalumu kwa kampuni za Tanzania katika zabuni za ndani na za kimataifa.
Pia sheria hiyo itaongeza ufanisi na kupata thamani halisi ya fedha, inayotumika kwa kununua huduma na bidhaa.
Dk Mpango alisema pamoja na kuongeza uwajibikaji, sheria hiyo mpya itapunguza vikao vya bodi hadi kuwa kimoja kwa robo mwaka na vikao vya dharura, kufanyika pale ambapo mwenyekiti ataona inabidi.
Pamoja na maelekezo hayo mapya, serikali pia itaanza kununua bidhaa na huduma kwa bei inayoendana na bei ya soko, iwapo wabunge watapitisha marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Pamoja na ununuzi wa bei ya soko, sheria mpya imelenga kuweka sharti la kisheria kutoa upendeleo katika zabuni mbalimbali, hasa kwa makundi maalumu kama vile wanawake, vijana, wazee na watu wenye mahitaji maalumu.
Alieleza kuwa sheria mpya imelenga kuiwezesha serikali, kunufaika na matumizi ya viwango na kuweka sharti la kisheria la kutumia mifumo ya kuongeza uwazi katika ununuzi ili kuongeza uadilifu na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa waziri, sheria mpya imelenga kurahisisha ununuzi wa umma na kuipa faida serikali baada ya kuwapo kwa changamoto nyingi kwa Sheria Namba 7 ya Mwaka 2011, ambayo ilianza kutekelezwa mwaka huo.
Changamoto hizo ni pamoja na bei ya juu ya bidhaa na huduma zinazonunuliwa na serikali kulinganisha na bei ya soko kutokana na zuio la majadiliano kuhusu bei kati ya taasisi nunuzi na mzabuni.
Pamoja na changamoto ya bei, kumekuwepo na muda mrefu wa mchakato, gharama kubwa zinazotokana na matangazo na vikao mbalimbali vya kupitia zabuni, kutozingatiwa kwa viwango na kutokuwepo kwa upendeleo katika ushiriki wa zabuni kwa makundi maalumu.
Mapendekezo ya muswada huo, pia yametaka pale kampuni au taasisi ya umma inapolazimika kufanya ununuzi kutoka nje ya nchi, hasa kama ni suala la ushauri linafanywa na kampuni ya nje ya nchi, ofisi hiyo ya serikali inalazimika kuhakikisha kuna wataalamu wa ndani ya nchi.
Aidha, kampuni au mshauri huyo wa nje ili apewe zabuni katika shughuli ambazo zinagharimiwa na fedha za umma, kuna kigezo cha kuhakikisha wafanyakazi wa kampuni yake, zaidi ya asilimia 60 ni Watanzania.
Mbali na kuwa na asilimia 60 ya wafanyakazi Watanzania, kampuni husika lazima ieleze kiwango cha bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi, ambazo itazinunua katika utekelezaji wa shughuli zake.
Nayo Kamati ya Bunge ya Bajeti imeitaka serikali kusimamia na kuhakikisha kwamba watumishi wa umma ambao hawastahili kupewa magari, watumie magari yao binafsi ; na wale ambao wanastahili wakopeshwe magari na serikali na kupewa posho kidogo kwa ajili ya mafuta na matengenezo.
Pia, imeitaka serikali iandae utaratibu wa kununua magari kwa pamoja yasiyo na gharama kubwa kulingana na bei ya soko.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Ghasia alisema kamati imekubaliana na serikali kufanya manunuzi kwa kuzingatia thamani ya fedha kwa bidhaa, ikiwamo manunuzi ya magari
Alisema muswada huo unaonesha kwamba inawezekana kupunguza gharama za serikali kwa kufuata thamani ya fedha.
Aidha kamati hiyo imeishauri serikali kuanzisha mfuko wa uwezeshaji wa makandarasi ili waweze kumudu utoaji wa huduma mbalimbali, zinazohuisha gharama kubwa, mfano ukandarasi wa barabara.
Mfuko huo utakuwa ukitoa dhamana. Pia kamati hiyo inataka kujua mwanzo wa matumizi ya sheria mpya.
Wabunge waliochangia muswada huo, waliitaka serikali nayo kujiunga katika sheria hiyo kwa kuona kwamba inawalipa wazabuni mapema au inaeleza watakavyoweza kuwa wazabuni wanapochelewesha malipo, hasa kutokana na kampeni yake ya ununuzi kwa bei ya soko.
Wabunge hao walisema kwamba serikali inajua sababu za bei kubwa na hivyo inafaa ikajipanga kuondoa kasoro hiyo ili hiyo sheria iweze kutekelezeka.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Ligora (CCM) alitoa tahadhari kwamba sheria inabadilishwa Ibara 40 ambayo ni sehemu kubwa na kusema kwamba lazima ijiandae kuondoa sababu za bei kubwa na pia kutofuta kipengele cha kamati ya mipango na fedha kwenye halmashauri kupitia zabuni kwa lengo la kujiridhisha.
Kauli ya kutofuta kipengele hicho katika muswada, pia ilizungumzwa na wabunge waliochangia jana.
Aidha wengine walitaka kuwapo na dirisha kwa ajili ya dharura na hasa dirisha kwa ajili ya bidhaa za afya na tiba. Wabunge wengine waliochangia ni Martha Mlata, Rita Kabati, Ali Hassan, Dk Diodorus Kamara, Japhet Asunga, Adadi Rajab, Jitu Son, John Kadutu na Amina Mollel.
No comments:
Post a Comment