Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema hawatakubaliana na kauli ya Rais John Magufuli ya kukataza mikutano ya shughuli za siasa hadi mwaka 2020 na kama hivyo ndivyo, Serikali iandae magereza ya kutosha.
Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema jana kuwa kutokana na kauli hiyo kuwa nzito vyama vinavyounda umoja huo vitakutana na kujadiliana kabla ya kutoa msimamo wa pamoja.
Mbunge huyo wa Hai alisema wamepokea kwa mshtuko mkubwa kauli na maagizo ya Rais Magufuli kuhusiana na haki ya kufanya shughuli za kisiasa ikiwamo mikutano ya hadhara, makongamano na hata maandamano kwa vyama vya siasa.
“Aandae magereza ya kutosha kwa sababu hatutazibwa midomo... kama wananchi wananyimwa fursa ya kusema ni vibaya, watatumia vitendo mambo ambayo yalileta vita katika nchi za wenzetu.
"Mbowe alisema Rais Magufuli anastahili kujua siasa siyo starehe, bali ni kazi kama zilivyo nyingine zozote. Alisema siasa siyo tukio la uchaguzi, bali ni maisha ya kila siku na ni mfumo unaogusa maisha ya kila siku.
"Mbowe alisema Rais Magufuli anastahili kujua siasa siyo starehe, bali ni kazi kama zilivyo nyingine zozote. Alisema siasa siyo tukio la uchaguzi, bali ni maisha ya kila siku na ni mfumo unaogusa maisha ya kila siku.
“Uhalali wa kazi za siasa unatolewa na Katiba aliyoapa kuilinda na kukaziwa na Sheria Namba 5 ya mwaka 1992 (Political Parties Act NO. 5 of 1992) pamoja na marekebisho yake,” alisema.
Alisema uhalali huo ndiyo unaomfanya yeye kuwa Rais leo na ndiyo unaotoa uhalali wa chama chake kuwepo na kutekeleza kihalali na kisheria majukumu yake ya kila siku.
Alisema haki ya kufanya siasa haiwezi kuwa miliki ya Serikali, wabunge na madiwani pekee kama Rais anavyoagiza.
“Akumbuke uchaguzi mkuu siyo tukio pekee la kisiasa. Kuna chaguzi za serikali za mitaa, chaguzi za marudio na mambo mengine mengi. Ni wajibu wa msingi wa vyama vya siasa kufuatilia utendaji kazi wa kila siku kwa wale wanaoongoza Serikali na hivyo siasa siyo uchaguzi pekee,” alisema Mbowe.
Alisema elimu ya uraia na ile ya siasa ni wajibu mkuu wa vyama vya siasa na hustahili kutolewa wakati wote na siyo na wanasiasa wa kuchaguliwa au kuteuliwa pekee.
“(Rais Magufuli) anapaswa kubaini kuwa vyama vya siasa vina miundo ya viongozi na watendaji nchi nzima ambao majukumu yao ni ya muda wote na siyo ya msimu wa uchaguzi pekee,” alisema.
Alisema makongamano yakiwamo ya siasa anayolalamikia Rais ni pamoja na Kigoda cha Mwalimu J.K. Nyerere ambalo lilionekana kuhoji mambo kadhaa yanayogusa mustakabali wa nchi.
“Makongamano katika vyuo na taasisi mbalimbali ni sehemu muhimu ya taaluma na huibua uelewa muhimu kwa jamii,” alisema.
Alisema makongamano mengi huandaliwa na taasisi zisizo za kiserikali na taasisi za dini na kusema Rais anastahili kutambua kuwa siasa inamgusa kila mmoja kwani ni maisha ya watu.
Mbowe alisema; “walianza kwa kulithibiti Bunge na wabunge wa upinzani kwa kujaza askari bungeni kama vile ni uwanja wa vita. Leo ni vyama vya siasa vya upinzani kupewa likizo ya lazima ya Rais; kesho inaweza ikawa taasisi za dini, baadaye asasi zisizokuwa za kiserikali na hatimaye nchi hii itaweza kugeuka nchi ya utawala wa mabavu ya kutumia dola,” alisema na kuongeza:
“Ukawa hatutakubaliana na hali hii. Hili ni tamko la hatari kwa demokrasia, utawala wa sheria, haki za binadamu na linakinzana na kila aina ya uhuru ambao Katiba yetu aliyoapa kuilinda Rais, imetoa.”
Aliwataka Watanzania wote wakatae utamaduni huu mpya ambao alisema utabomoa mshikamano wetu kama Taifa.
Mbowe alisema Rais kuwa mkali katika kusimamia uwajibikaji na utendaji wa Serikali ni jambo jema lakini linapoteza maana kama ukali huo unatumika kuvunja Katiba na sheria na kuziba watu midomo.
Mbowe alisema Rais kuwa mkali katika kusimamia uwajibikaji na utendaji wa Serikali ni jambo jema lakini linapoteza maana kama ukali huo unatumika kuvunja Katiba na sheria na kuziba watu midomo.
“Uhuru ni jambo la kupigania na kutetea kwa gharama yoyote ile na tuko tayari kwa wajibu huo. Wanaoweza kumshauri Rais na wafanye hivyo kwani athari za jambo hili likiachiwa likaota mizizi, hata hayo maendeleo anayoyapigania yanaweza kubaki kuwa ndoto na nchi kuingizwa kwenye machafuko yasiyo ya lazima,” alisema.
James Mbatia
Msimamo kama huo pia ulitolewa na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia aliyesema Rais ameweka kando Katiba.
Msimamo kama huo pia ulitolewa na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia aliyesema Rais ameweka kando Katiba.
Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo (NCCR- Mageuzi), alisema kauli nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa na Rais zimekuwa hazizai matunda na kutoa mfano wa kuzuia sukari kutoka nje ya nchi kuingia nchini jambo ambalo muda mfupi baadaye, ilibainika kuwa sukari ya nchini haitoshelezi mahitaji.
“Hatuombi ruhusa kwa Rais kufanya mikutano ya kisiasa, bali ni haki yetu kikatiba,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Riziki Ng’wale, alisema kauli ya Rais Magufuli si sahihi kwa sababu siasa ni kazi na hakuna namna anavyoweza kuweka wigo wa kuyafanya mambo hayo.
“Kwa sisi wakongwe wa siasa tunamwambia apanue magereza, hatutakubali hilo... Aache ubabe,” alisema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini, (ASA), Paul Louslie alisema agizo la Rais Magufuli ni gumu kutekelezeka hata ndani ya CCM.
“Kukaa bila kukutana kwa vyama vya siasa hata ndani ya CCM labda kwa sababu yeye ni Mwenyekiti wa CCM na ni Amiri Jeshi Mkuu. Na hapo akiamua kutumia madaraka yake hatatenda haki kwa vyama vingine vya kisiasa,” alisema.
Alisema kazi ya siasa ni kukutana na watu na haiwezekani kukaa ndani bila kukutana na watu kwa muda wote kwani huko ni kuua chama.
No comments:
Post a Comment