Thursday 2 June 2016

Waziri Muhongo azungumza haya kuhusu nishati ya uhakika katika kuinua viwanda nchini.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema ili Tanzania iwe nchi ya viwanda, nishati ya uhakika inahitajika na kutaka kampuni kuwekeza katika uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi.

Aliyasema hayo Dar es Salaam katika nyakati tofauti alipokutana na watendaji wa kampuni zinazojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi na wataalamu wake na wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), lengo likiwa ni kupokea taarifa ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya kampuni hizo.

Kampuni hizo zinazofanya kazi kwa kushirikiana na TPDC ni British Gas (BG), Ophir, ExxonMobil na Statoil. Alisema hakuna nchi yoyote duniani iliyopiga hatua kimaendeleo bila kuwa na nishati ya uhakika ya umeme na kuwataka wawekezaji kuchangamkia fursa kupitia gesi nyingi iliyogunduliwa.

Alitaja maeneo yanayohitaji uwekezaji katika kuzalisha umeme kwa kutumia gesi kuwa ni Mtwara, Lindi, Somanga Fungu na Mkuranga. Aliongeza kuwa viwanda 37 na vya saruji vinahitaji gesi na kusisitiza kuwa iwapo sekta ya gesi itatumiwa ipasavyo inaweza kuchangia nchi kupiga hatua na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyosema.

No comments:

Post a Comment